RIWAYA: MCHEZO WA JOGOO (sehemu ya pili)
Wanaume sita walioshiba misuli walikuwa
ndani. Mumewe Mayasa alikuwa miongoni mwao, huyu ndiye aliyekuwa na hasira
kuliko wote. Mzee Chekeche aliweza kuwatambua watu wawili, mumewe Mayasa na Bwana
Mashiri. Siku tatu tu zilizopita mzee Chekeche alifumaniwa na mke wa Mashiri.
Mashiri akamwacha mzee aondoke lakini akavunja ndoa, Mashiri naye alionekana
kushiba hasira.
“Mume
wangu nisamehe…” alijitetea Mayasa.
“Nikusamehe
kitu gani, mwanamke huna aibu unazini mchana kweupe bila kuogopa tena na hiki
kizee kilichochoka.”
“Tafadhali
kijana nitake radhi, sijachoka mie…” alilalama mzee Chekeche. Mumewe Mayasa
akapata hasira akamsogelea mzee na kumpiga kofi moja zito la uso, mzee
akamsukuma, akakimbia kuliko mlango, huko akakutana na wanaume watano,
wakajaribu kumdhibiti, akawa mbishi, wakampiga ngumi nyingi lakini hatimaye
kulingana na uzoefu wa uzinifu wa mzee huyu alifanikiwa kuufikia mlango akiwa
amepigwa haswa, mlango wenyewe ulikwisha jeruhiwa hakupata shida, punde tu
alikuwa nje, akakimbia kwa mwendo wa farasi akiwa haamini kama kaponyoka kwenye
fumanizi lile.
Mzee Chekeche akiwa na kaptura yake
nyepesi, hana shati kifua kiko wazi alikimbia mpaka nje, watu walishangaa
lakini hakujali, aliitoka Nyambizi guest house, akaibukia katika barabara ya
Mtaka shari, kabla hajaivuka gari dogo lililokuwa kasi likataka kumgonga lakini
dada aliyeliendesha alimudu kuzifunga breki na kulifanya liserereke na kuacha
harufu ya matairi.
“We mzee mchawi nini?” alihoji dada.
“Binti
yangu nisaidie nipe ‘lift’ kuna watu wabaya wanaiwinda roho yangu… nisaidie
nitakusimulia.
Binti hakuwa mtu wa hiyana wala maswali
mengimengi, aliufungua mlango wa mbele wa gari lake, mzee Chekeche akaingia na
kukaa pembezoni mwa dereva. Kwa vile mzee hakuwa na shati binti alifunga
madirisha yaliyokuwa na uwezo wa kuzuia watu wa nje kuwaona waliokuwa ndani.
Japokuwa kioo cha mbele kiliweza kuonesha, binti hakujali… akazikanyaga pedali
gari likatembea tena.
Itaendelea Jumapili...