Kiswahili pre NECTA 4

Gari ikitimua vumbi
Jibu maswali yote;
SEHEMU A (alama 10)
1.   Soma kifungu cha habari ifuatayo kisha jibu maswali kama ilivyoelekezwa.
Mako, mwosha magari maarufu mtaani Sakubimbi, alishughulika kama kawaida yake. Leo alionekana kuchoka zaidi, pengine tenda ya kuosha Fuso, ilimnyong’onyeza vilivyo. Mwanaume huyu alikuwa na mwili wa wastani tu, kakamavu aliyezifikia kilo 61 kwenye uzani.
     Wakati akiendelea kuosha Fuso ile, jua liliendelea kuipiga ngozi yake, naye hakuisha kushika nywele, kipilipili kilichokoza, ngumu zimerundikana na kutengeneza kitu kama mkutano wa nzi, labda hazikuliona chanuo kwa muda!
     Fuso sasa ilitakata haswaa, Mako akatembea mpaka alipo mwajiri wake, akachukua fedha na kuzielekeza kibindoni, kabla hazijafika akastushwa na sauti yenye kitetemeshi cha kuigiza,
     “Uko chini ya ulinzi, toa fedha uishi…”
Mako akabinua bichwa ili apate kumtazama aliyetema maneno hayo, macho yake yakagongana na sura ya mtoto mdogo, umri miaka saba, kavaa sare za shule na begi dogo kalipachika mgongoni, kisha akambeba kindakindaki. Kwa ambae angewaona hata kama angekuwa mgeni eneo hilo ni lazima angegundua kuwa viumbe wale walikuwa ni mtu na mwanae. Nkenye alifanana mno na baba yake, hasa zile nywele, kipilipili kilichokoza. Majirani walisema Nkenye alijaa urumbi wa maneno kama babaye.

MASWALI

i.             Andika kichwa cha habari hiyo kwa maneno yasiyopungua matano.
ii.            Ni kazi gani alifanya Mako?
iii.           Nini maana ya neno kibindoni?
iv.          Kwa nini watu walisema kuwa Mako alifanana na mwanaye?
v.           Taja mafunzo mawili yanayopatikana katika habari hiyo?

2.   Andika ufupisho wa aya ya mwisho kwa maneno yasiyozidi 30.

SEHEMU B (alama 25)

3.   Katika kila moja ya sentensi zifuatazo, onesha kosa moja la kisarufi kisha andika sentensi hiyo kwa usahihi.
a)     Kinyonga kinakimbia. b) Arusi ya dada yenu zitakuwa Disemba 2015.
c)   Mwaka huu jua zinachoma sana. D) Tafadhali nikope shilingi mia nitakurudishia kesho kutwa.
e)   Kichumba hiki kichafu sana.
4.   Onesha dhima ya kiambishi “ni” kilichopigiwa msitari katika sentensi zifuatazo.
a. alinisaidia b. wajumbe wapo mkutanoni
c.wakubalieni d. yeye ni mvivu e.  nina kalamu

SEHEMU C (alama 10)

5.   Eleza tofauti iliyopo kati ya hotuba na risala. Andika hotuba kuhusu “Maji ni Uhai.”

SEHEMU D (alama 10)

6.   Eleza jinsi shughuli za Waarabu zilivyosaidia kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili nchini Tanzania kabla ya uhuru.

SEHEMU E (alama 45)

7.   “mwandishi wa fasihi ni mchunguzi wa jamii ambaye huyaweka wazi maovu mbalimbali”. Jadili jinsi kazi za washairi wawili kati ya hao walioorodheshwa zilivyosadifu kauli hii.
8.   “Msanii ni mwalimu wa jamii”. Thibitisha kauli hii kwa kutumia riwaya mbili ulizosoma.

9.   Tunga utenzi wenye beti nne kuhusu umuhimu wa maji.Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne