BANGI NYINGI! KONA NYINGI! GIA NYINGI! MWENDO TU!
Walimuita dereva Kankono! Mkono wa
kulia ulipinda kidogo kutokana na ajali kadhaa za gari alizopata kutokana na
udereva wake wa pupa! Ila watu walimpenda, walisema, ukipanda gari lake wala
makalio hayaumi, sekunde tu, unafika uendako. Waliojaribu kuhoji zaidi
waliambiwa kufa kupo tu, kama siku yako imepangwa huwezi kwepa! AKILI NDOGO
ZILIFIKIRI KIDOGO.
Jana kabla ya safari, dereva
Kankono, alifanya maandalizi ya kutosha. Alianza kwa kuvuta bangi ya miatisa
kisha akamalizia kwa kunywa bia saba. Akawa ‘fit’ tayari kabisa kukaa nyuma ya
usukani.
Alipoliwasha gari abiria
walishangilia! “woyoooooh.” Kankono akafurahi. Haraka sana akakanyaga ‘krach’
akapachika gia ya kwanza, ‘krach’ gia ya pili, ‘krach’ gia ya tatu… mayowe
yakaongezeka, Kankono akamaliza gia zote, ‘at their own risk.’
Gari lilikimbia kilomita 117 kwa saa
katika barabara mbovu yenye kona nyingi. Kankono hakujali, badala yake akiwa
katika mwendo huo, alichukua kilo moja ya mirungi akaanza kutafuna kama beberu
la mbuzi. Alipomaliza mirungi, akachukua kikopo cha ugoro, akaanza kwa kunusa,
akapiga chafya nene, gari likayumba, watu wakashangilia, “woyooooh.” Akiisha
kuachana na kikopo cha ugoro, akaamua kutuliza mawazo yake ili aendelee na
safari!
Mara ghafla kona kali, akajitahidi
akaikwepa na kuongeza mwendo mpaka kilomita 129 kwa saa! kona
ya pili akapita ila gari likalala kidogo, kona ya tatu gari likayumba, kona ya
nne gari likaacha njia kisha likagonga mti mkubwa wa mbuyu. NITAKUWA MWONGO
NIKISEMA KUNA MTU ALIPONA.