SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya tano)
Tulipofika uwanjani tulicheza mpira na mwana mfalme,
kuna wakati alinigusa nikaumia, akanipa pole, mchezo ukaendelea. Hakuna mtu
angeweza kuamini kuwa ni siku hiyohiyo nilikuwa nimedondoka katika chombo cha
anga kwa jinsi nilivyokuwa na nguvu na furaha, lakini sikusahau kile
nilichotumwa.
Tulicheza mpira mpaka mwana mfalme aliponambia ya
kwamba usiku umeingia, tukaacha mchezo
na kuelekea nyumbani.
Tulifika katika meza ya mfalme, tukamkuta mfalme
amekaa na watu ambao sikuwafahamu, Mwanamfalme akanambia ya kwamba ulikuwa ni
muda wa chakula, hivyo nilikaa katika kiti kimojawapo.
Nilipewa karai kubwa la chakula, ndani ya karai lile
paliwekwa mawe, mchanga na kokoto. Bila shaka hiki ndicho chakula nilichotakiwa
kula!
Mfalme alishtuka baada ya kuona sili chakula kile,
kisha kama aliyetoka usingizini akakumbuka ya kuwa mwanadamu toka Duniani huwa
haishi kwa kula mawe.
“Jamani tutafanya nini? Mwanadamu hawezi kula mawe!”
alisema mfalme, mzee mmoja aliyekaa upande wake wa kushoto akajibu,
“Mnakumbuka kuhusu upembe wa shaba unaomilikiwa na
binti waziri wa fujo na mikasa?”
Wote walitikisa vichwa kukubali. Mzee akaendelea
kuzungumza.
“Basi upembe ule huweza kutoa chakula cha aina
yoyote.”
Askari wawili walitumwa kwenda kumuita binti waziri
usiku uleule, mfalme alinijali sana na hakutaka kabisa nisumbuliwe na njaa.
Baada ya masaa matatu, binti waziri alifika akiwa ameuvalia shingoni upembe
wake wa shaba. Mate ya hamu ya chakula yakaanza kunidondoka, nilitamani
kumrukia binti waziri niuamrishe upembe unipe chakula lakini nilivuta subira.
Binti waziri alisalimiana na mfalme, mfalme akamweleza
yote yaliyonisibu na kwamba tegemeo pekee la mimi kupata chakula ulikuwa ni ule
upembe.
“Mwanadamu, puliza upembe huu kisha taja jina la
chakula unachotaka… punde kitakuwa mezani.” Aliniamuru binti waziri kisha
akanipatia upembe.
“Vuuuuuuuh!” niliupuliza upembe kisha haraka nikasema,
“Nataka wali wa kushiba na nyama ya kuku, mchuzi mwingi.”
Itaendelea Jumapili...