SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya sita)
Looh kabla hata sijamaliza kusema, wali na nyama ya
kuku ulikuwa mezani. Nilikula haraka haraka huku watu wote wakinishangaa,
sikuwajali, kwa njaa niliyokuwa nayo, nilistahili kula hivyo.
Wakati nikiendelea kula, kuna jambo lilinishangaza,
binti waziri alikuwa akiteta jambo na mfalme, huku wakinitazama sana.
Nilipotazama pembeni sikumuona rafiki yangu Chokusi. Nikahisi hatari kubwa
ilikuwa ikininyemelea.
Niliendelea kula nikiwa na mashaka, mpaka chakula
chote nikakimaliza. Mfalme akanitaka nikalale, pia akanieleza ya kwamba kesho
alikuwa na mazungumzo muhimu sana na mimi. Nilikubali kisha nikajikokota katika
chumba kilichokuwa jirani, humo nilimkuta mwana mfalme Chokusi amekwisha lala.
Nikaungana naye.
Asubuhi niliamshwa na Chokusi, akaniomba tukacheze
mpira wakati tukisubiri chai. Hapo nikagundua ya kwamba nchi hii watu wake
hawapigi mswaki.
“Aaah, mfalme alisema anataka kuzungumza nami, hivyo
nisindikize kwanza nikamuone.” Nilimjibu Chokusi, haraka akanisindikiza mpaka alipokaa
mfalme.
Tulifika na kumkuta mfalme akiwa amevalia mavazi
meupe, pembeni yake alikaa binti waziri, shingoni akiwa kauning’iniza upembe wa
shaba! Mtu wa tatu alikuwa yule mzee wa jana aliyetoa habari za binti waziri.
Niliruhusiwa kukaa katika kiti kimojawapo, Chokusi
akaambiwa apishe, naye akatii kwa adabu. Nikiwa nimekaa mfalme akaanza
kuzungumza nami.
“Mwanadamu sisi ni viumbe wema kwako, tumekusaidia
nawe sasa ni zamu yako kutusaidia. Kuna hazina ya vitabu muhimu sana vya
mafanikio vilifichwa nchi ya mbali, sehemu palipo vitabu hivi kuna sumaku kali
ambayo ndiyo sumu kwetu, viumbe wa chuma hunaswa na sumaku na huo huwa mwisho
wetu. Lakini wewe mwanadamu wa nyama, sumaku haina madhara kwako… tafadhali
tunaomba utusaidie kuvipata vitabu hivyo!”
Nilijua ni kazi rahisi tu, nikamjibu mfalme kuwa
nilikuwa tayari kwenda hata asubuhi ile. Mfalme akanijibu,
“Asante sana… lakini nilisema vitabu hivi vilifichwa
mbali sana, kufika huko sio safari ya siku moja, ni safari ya miaka tisa
kwenda, kwa hivyo itakuchukua miaka kumi na nane kwenda na kurudi!”
Taarifa hiyo ilinishtua sana, nikajikaza na kumweleza
mfalme,
“Haiwezekani… ndugu zangu hawawezi kuishi miaka kumi
na nane bila mwezi… ni lazima nikautafute mwezi wetu na kuurejesha nyumbani
mapema iwezekanavyo.”
Mzee aliyekuwa pembeni akafoka,
“Akisemacho
mfalme ni amri, huna haki ya kupinga… utake utakwenda usitake utakwenda.”
Baada ya mzee kutoa maneno makali, mfalme alinyanyuka
kisha bila kutegemea nilikamatwa na askari sita, wakanipeleka mpaka katika chumba kimoja kidogo kilichokuwa na giza kali
wakaniacha humo, nikiwa sina lolote la kufanya.
itaendelea jumapili...