SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya tatu)


Minza alitusalimu, kisha akakaa pembeni, sikutaka kupoteza Muda niliingia ndani ya Mapandagila 214, tayari kwa safari ya kuusaka mwezi.

Nilikaa ndani ya Mapandagila 214, nikaiwasha, ikaunguruma kama simba, nilitaka kuwaonesha kuwa mimi ni mtaalamu wa kuendesha Mapandagila ndani na nje ya nchi ya Lahaja. Taratibu nikairusha hewani, niliizungusha polepole katika uwanja ule wa nyumba ya mfalme, nikakunja kona na kuirusharusha kama mpira, halafu nikaitembeza kwa mwendo wa konakona mithili ya kiluwiluwi ndani ya maji, hapo nikaona mfalme na watu wake wakinipigia makofi. Sikutaka kulewa sifa, nikapiga gia kubwa, Mapandagila ikapaa juu, hapo nikatuma taarifa makao makuu,


            “Mapandagila inatembea mwendo wa sauti tisa za kunguru dume!”

Chombo kilikimbia kwa mwendo wa kasi mpaka kikaitoka Dunia. Nikasikia katika mtambo wangu wa mawasiliano watu wa makao makuu wakinipongeza kwa hatua hiyo. Nikatabasamu kwa ushindi mdogo nilioupata.

Lakini ghafla, nililiona jeshi la vichawi vya anga likinifuata kwa kasi,

            “Makao makuu jeshi la vichawi vya anga linanishambulia.” Nilituma taarifa.

            “Ongeza kasi, kimbia mwendo wa sauti 18 za kunguru dume.”

Niliongeza kasi kama nilivyoamuliwa, kwa mbali nikaliona kombora lililotumwa na vichawi vya anga, nikalikwepa, likarushwa kombora jingine, nikakwepa. Chombo changu kilijaa makombora mengi, lakini sikutaka kuyatumia kwani ilikwishaamuliwa kuwa zama za uadui zilikwishapita na mauaji hayakuwa na nafasi tena.

Vichawi vya anga vilikuwa vingi kama nyuki, viliendelea kunishambulia kwa makombora mazito nami niliendelea kuyakwepa makombora hayo, mpaka nilipokuja kupigwa kombora moja ambalo lilifanya mawasiliano yakatike, chombo kikayumba, nikashindwa kukiongoza kikanipeleka kule nisikotaka.

Chombo changu – Mapandagila 214 baada ya masaa saba ya kupoteza mwelekeo kilidondoka katika ardhi nisiyoifahamu, kikasababisha mshindo mkuu! Nikiwa nina hofu na nchi hii mpya niliamua kuimba wimbo wa kishujaa ili kupunguza wasiwasi.

            “Shujaa, kokote natua,
            Mojaa, namba naijua,
            Nitapambana, mpaka ushindi” niliimba wimbo huu mpaka niliposikia sauti ya mtu ikinitaka nitoke ndani ya Mapandagila 214. Nilifungua mlango nikatoka nikiwa na hamu ya kumuona kiumbe aliyegundua uwepo wangu.

Nilishtuka nilipomuona, alikuwa mrefu azipataye futi sita lakini hakuwa mtu wa kawaida, bali lilikuwa jitu la ajabu, tena jitu la chuma! Sikuwahi kumuona mtu aliyetengenezwa kwa chuma, nilishangaa sana, lakini kumbe wakati naendelea kumshangaa, naye alikuwa akinishangaa, hakuwahi kumuona mtu aliyetengenezwa kwa nyama!

            “We ni nani na umetoka wapi?” Aliniuliza kwa upole.

            “Nimetoka sayari inayoitwa Dunia, naelekea sayari iitwayo Vumu, huko nakwenda kuutafuta mwezi wetu ulioibwa na watu waishio huko.”

            “Chombo chako kimeharibika, hutaweza tena kupaa, twende ukapumzike mpaka pale kitakapotengenezwa.”

Nilikubaliana naye, akainyanyanyua Mapandagila 214 na kuibeba kama mtu mzima abebavyo ndoo ya maji, nilistaajabu sana nguvu za jitu hili la chuma.

Tukiwa njiani kuelekea katika mji wa jitu hili, nilijitahidi kuuliza maswali.

Itaendelea jumapili...

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne