Fomati Mpya Kidato cha Sita, Mambo ya Kuzingatia Ili Ufaulu

Fomati mpya kidato cha sita
Dereva wa daladala alikaa nyuma ya usukani, mkononi kashika sigareti, akavuta mkupuo mmoja, moshi ukaenda ndani, mapafu yakateketea!
Nami nilikaa katika siti ya daladala, hata hivyo nilikalia kipande kidogo cha siti kwa sababu nafasi kubwa ilimalizwa na jirani yangu aliyekuwa mnene kupitiliza. Nilipiga hesabu nikagundua, mimi na mifupa yangu, ningeingia mara tisa katika mwili ule!
Gari ikiwa katika mwendo ilipiga tuta, jirani yangu akanesa kisha akajaa zaidi, nikawa sasa nimebaki na nafasi ndogo ambayo sikuelewa kama nilikaa ama nilichuchumaa. Walimu tunapata shida sisi, ptuuuuuh!
“Mwalimu Makoba,” jirani yangu aliniita, nikashtuka.
“Unanifahamu? Uliniona wapi?” niliuliza nikimtazama kwa udadisi.
“Nakufahamu, nilikuona gugo,” alijibu.
“Sawa, una jina?” niliuliza.
“Ndiyo, ninalo, naitwa Tom Tom.” alijibu, kisha akaendelea, “lakini mwalimu, kwa nini wamebadili fomati? Kwa nini wafanye hivi tukiwa tumebakiwa na miezi michache tu, fomati yenyewe ngumu, ni kama maswali yote yamekuwa ya lazima.”
Baada ya kuhakikisha kuwa kamaliza maswali yake, nilijisogeza kidogo ili nikae vizuri, hata hivyo sikupata nafasi, nilibaki vilevile nisiyejua kama nimekaa ama nimechuchumaa, nikamjibu Tom Tom kwa maelezo marefu:
“Nakupa tahadhari Tom Tom, ukiichukia fomati hii, kuna uwezekano mkubwa wa kushidwa mtihani wako, ni lazima uipende, vyovyote vile lazima uipende. Kilichobadilika ni idadi ya maswali pekee, siyo mada, hivyo hakuna tatizo kwa mwanafunzi aliyesoma vizuri.
Mambo ya Kuzingatia ili Ufaulu Mtihani wa Fomati Mpya
1. Ipende fomati mpya
Usijaribu kuichukia, tafuta sababu za kuipenda. Miongoni mwa sababu hizo ni kwamba, fomati hii ina maswali machache hivyo ni rahisi kusoma maswali yote na kuchagua maswali unayotaka bila kupoteza muda mwingi.
2. Soma mada zote
Usiache mada hata moja. Katika fomati hii mpya, maswali mengi ni ya lazima na ya hiari hayazidi mawili, na mitihani mingine swali la hiari ni moja tu. Hivyo, kuna hatari ya kupoteza alama endapo hukusoma mada zote.
Pia, katika somo la fasihi, usisome vitabu viwiliviwili pekee. Soma vitabu vingi zaidi. Mfano: katika riwaya soma riwaya nne, ushairi soma diwani nne, nazo tamthiliya soma nne. Nasema hivyo kwa sababu kuna kipengele cha maswali mafupi, unaweza kuulizwa swali kuhusu kitabu chochote!”
Wakati nataka kuongeza hoja ya tatu, niligundua kuwa, Tom Tom alikuwa kasinzia naye hanisikilizi tena. Nilisimama nikamwamrisha konda,
“Nishushe kituo kinachofuata. Nauli atalipa yule Tipwa Tipwa aliyelala.”

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie