Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Utanitambua 3 | Riwaya

Mwanaume akivuta sigara
Na: Mwalimu Makoba

Baada ya mazungumzo marefu, Lightness aliondoka nyumbani kwa Mako. Mwanamume akabaki akiwaza juu ya kazi ngumu aliyotakiwa kuifanya.
“Nimefanya kazi nyingi zilizoikomboa nchi hii, lakini kila nikimaliza tatizo, hakuna anayenikumbuka, wanasherekea wenyewe na kupeana sifa katika karamu za kifahari. Mimi hukumbukwa tena pindi litokeapo tatizo,” Mako aliwaza peke yake.
“Hata hivyo nchi ipo katika hali mbaya kwa sasa, siwezi kukaa kimya, huu ni usaliti kwa nchi yangu, lazima niwashikishe adabu wapuuzi wote wanaonyanyasa wanyonge,” Mako alihitimisha mawazo yake. Awazapo namna hii, kazi kubwa huanza.
Haraka alinyanyuka katika sofa, akarusha mateke na ngumi mfululizo mpaka alipohisi yupo sawa kwa mapambano. Mwenye uchungu na nchi yake, alikisogeza pembeni kitanda, kisha akafunua chini katika sakafu, humo alificha siraha zake nyingi za maangamizi. Aliamua kuchukua siraha mojawapo, bunduki ya kisasa, Norinco 97, akaifuta vumbi na kuirudisha pahala pake. Alipomaliza ukaguzi wa siraha, akapanga kila kitu kama kilivyokuwa awali, kisha akachukua simu yake na kumwandikia ujumbe mfupi Lightness, “kazi imeanza.”
Nchi ya Andalasu ilikuwa katika shida kubwa. Mgodi pekee uliotegemewa na taifa hili masikini, ulivamiwa na kundi la wanyang’anyi waliokuwa na siraha za moto. Haikufahamika, ni nani alikuwa nyuma ya kundi hili. Kwa kuwa mgodi huu unaotoa Almasi kwa wingi kuliko mgodi wowote ule Duniani ulikuwa mikononi mwa wanyang’anyi, serikali ilipoteza fedha nyingi na ilianza kushindwa kujiendesha, hali ilikuwa mbaya katika serikali na uchumi wa nchi nzima.

Bofya Hapa Kujiunga Kundi la Riwaya za Mwalimu Makoba WhatsApp
Mgodi ulipotekwa mara ya kwanza, kilitumwa kikosi cha askari kwenda kuukomboa, askari wote waliuawa. Baada ya hapo kikatumwa kikosi cha makomando, ambacho nacho kilifyekelewa mbali na hakuna aliyebaki. Vikosi vingi viliendelea kutumwa na matokeo yalikuwa yaleyale, hakuna aliyerudi akiwa hai. Serikali ikawa katika hofu kubwa ya wanyang’anyi hawa wasiofahamika.
Vikosi vingine vilipotumwa kwenda kupambana na wanyang’anyi hawa, vilikataa kwa kutoa sababu kuwa, silaha walizotumia wao zilikuwa za kiwango cha chini mno ukilinganisha na wanyang’anyi ambao wao walitumia silaha kali zaidi. Wakati askari wa serikali wakienda kuvamia wakiwa na siraha aina ya SMG yenye uwezo wa kubeba risasi 30, wanyang’anyi walitumia siraha za maangamizi kama IWI X95 TAVOR ambayo iliweza kupiga risasi 950 kwa dakika! Mwenye nguvu mpishe.
Baada ya kuonekana kushindwa kwa vikosi vya serikali, suluhisho pekee lilikuwa kwa Mako, walimfahamu kwa sababu amesaidia mambo mengi akiwa raia mwema tu. Walipotazama matukio makubwa aliyoyafanya, wakaamini anawafaa, ndipo kwa kasi ya radi juhudi za kuanza kumshawishi zikaanza na mpaka sasa, Mako kakubali na yuko tayari kupambana.
Katika chumba alichokaa Mako mlio wa risasi ulisikika. Isingekuwa wepesi wake wa kudondoka chini, risasi ile ingelipasua fuvu lake na kumfanya atupwe katika shimo la sahau. Aliyetumwa kufanya mauaji yale alimtambua vyema Mako, alipoona kamkosa alifahamu nini kingefuata. Hakutaka kuhangaika, akakimbia.
Mako alimwona kijana yule akikimbia, alitoka na kuanza kumfuatilia taratibu ili ajue alikokwenda. Kijana alikata kona na kuingia barabara ya dhiki, hapo ndipo aliegesha gari yake. Wakati anaondoka, Mako alikodi baiskeli kwa mfanyabiashara mmoja aliyekuwa anakodisha baiskeli eneo hilo. Gari ikawa mbele, na Mako akawa nyuma na baiskeli yake, aliacha umbali mkubwa ili kuepuka kuonekana.
Gari liliingia barabara ya Matumaini, kisha likakunja kona na kuyafikia makazi ya Uzitoni. Inasemekana katika jiji la Igaga, Uzitoni ndipo walikaa watu. Kijana aliendesha na kushuka katika nyumba ya kifahari, aliingia humo na hakutoka kwa wakati huo. Mako aliitambua nyumba ile, ilikuwa nyumba ya Mwanamama tajiri na waziri wa madini na ardhi, Ramona Fundikila.
Itaendelea Jumapili...


Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne