Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Utanitambua 2| Riwaya

mtu katika giza
Majambazi wale walitaka fedha. Kwanza walitaka kuchukua fedha kwa wahudumu waliokuwa wakiuza vinywaji, kisha warudi kwa watu kila mmoja aweke kiasi alichokuwa nacho. Mako alilitambua hilo, akatabasamu kama kitoto cha mamba.
Mako alimwomba Lightness atulie, kisha akatambaa taratibu bila kuonekana mpaka sehemu palipouzwa vinywaji, alipofika, akatega pale mithili ya chatu mwenye njaa.
Jambazi aliyekuwa na siraha, akaanza kutembea kuelekea sehemu palipouzwa vinywaji ili kuchukua fedha, alipofika mahali pa kuingilia, Mako akamvuta miguu yake na kumwangusha chini, haraka akampokonya bastola yake. Mwenzake kule mbele akataka kukimbia, Mako akamtandika risasi ya mguu akadondoka chini akigugumia maumivu. Watu walipoona Mako anapambana na mpambano kauweza, wakawakamata wale majambazi wasio na bahati wakitaka kuwashushia kipigo. Mako kuona hivyo akanena, “Jamani, muda uliobaki ni kidogo sana, tukianza kuwapiga hawa, asubuhi itafika hatujacheza mziki, mimi naomba mabaunsa watusaidie kuwapeleka polisi waharifu hawa. Sisi tuendelee kucheza muziki.
Watu wakashangilia kukubaliana na hoja ya Mako, muziki ukawashwa, Lightness akasogea alipo Mako, nyonga ikaendelea kuzungushwa. Hata hivyo watu walicheza mbali kidogo na Mako, walimwogopa, ni binti mmoja tu ambaye hakumhofia Mako, Lightness!
Mako na Lightess walizama katika dansa mpaka ilipofika saa kumi usiku. Lightness alikuwa kanyong’onyea asiyeweza tena kusimama. Mako alitambua haraka kuwa kilichomlegeza binti huyu ni kilevi alichotumia. Lengo lake lilikuwa kucheza naye tu kisha ifikapo asubuhi, arejee nyumbani. Sasa mambo yalikuwa tofauti, akawaza na kuwazua.
Mwisho Mako aliamua kuondoka na msichana yule kwani angemwacha mle huenda angebakwa. Lightness hakujitambua kabisa wakati huo. Mako akamkokota kama mkokoteni na wote wawili  wakatokomea katika vichochoro vya jiji la Igaga.
Mlango wa chumba ulifunguliwa, Mako akaingia akiwa kambeba mikononi Lightness. Alipoingia, akaufunga mlango kisha akamtupa kitandani Lightness. Baada ya kuwasha taa Mako aliuona uzuri wa umbo la msichana, hata hivyo akaamua kumshinda shetani, akalala katika sofa la watu wawili lililokuwa katika chumba kile.

Bofya Hapa Kujiunga Kundi la Riwaya za Mwalimu Makoba WhatsApp
Mako aliamka saa tano. Alipotazama pembeni, alimwona Lightness kakaa kitandani. Bila shaka binti huyu aliamka mapema sana.
“Sijawahi kuona mwanamume kama wewe!…” alizungumza Lightness, “nimejikagua sehemu zote, sijaona baya ulilonifanyia. Umewezaje?”
“Mapenzi haya raha bila ushirikiano. Pia kwa heshima niliyonayo katika jamii hii, ni aibu kubwa kuwa mbakaji.” alijibu Mako.
“Kuna supu nimekuandalia, chukua juu ya meza.”
Mako alishangaa, hata hivyo alinyanyuka na kuchukua supu aliyoandaliwa. Supu ilikuwa tamu na ilimpa nguvu tena.
“Shukrani sana, ni nani kakupeleka buchani?” aliuliza mako, akiweka chini mfupa wa mwisho.
“Nilikwenda mwenyewe, wajua ni vigumu mtaa kukosa bucha… hata sijahangaika ni hapo mbele.”
Mako alitabasamu, akachukua rimoti na kuwasha luninga iliyotundikwa ukutani. Hapo akachagua ‘channel’ iliyoonesha mpira.
“Lightness.” aliita Mako
“Naam…”
“Unatakiwa kwenda nyumbani sasa. Muda huu ni saa saba mchana, na ulisema jana umetoroka, hivyo naomba urejee kwenu, usiwape hofu.”
“Mako nimekuzoea ghafla, nitaondoka tu niache nikae kidogo, usinifukuze.”
Mako alishtushwa na jibu lile. Kama ni kulinunua balaa basi alilinunua. Kung’ang’aniwa na mwanamke uliyekutana naye ‘club’ kulimtisha Mako. Akatafakari mbinu ambazo zingemfanya Lightness aondoke nyumbani kwake.
“Mako, najua unatafakari mbinu za kunifanya niondoke kwa sababu hunifahamu!” alisema Lightness macho kamkazia Mako. “Tafadhali sana Mako naomba sana niko chini ya miguu yako. Naomba utusaidie, tusaidie sisi, isaidie nchi yako.”
Mako hakutarajia alichoambiwa. Alielewa maneno yale yalitoka wapi, lakini njia iliyotumika ilimshangaza.
“Wamekutuma uje kunibembeleza wakidhani mimi ni dhaifu kwa wanawake?” aliuliza Mako.
“Siyo hivyo Mako. Hali halisi ndiyo inasababisha yote haya. Bila matatizo tusingekuwa tunakufuata tena na tena, tunarudi mara zote kwa sababu lazima ufanye kazi hii.”
Mako anatakiwa kwa kazi gani? Itaendelea Jumapili...

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Sifa Bainifu za Irabu ya Kiswahili Sanifu