Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Utanitambua 1| Riwaya

mwanamume akiwa na hasira

Na: Mwalimu Makoba

Mako alikaa katika kiti cha kuzunguka ndani ya ‘night club’ moja katika jiji kubwa la Igaga. Hali ya hewa ya jiji hilo ni joto, lakini ndani ya kiota hicho cha burudani, kulikuwa baridi kwa sababu ya vipupwe vya kisasa vilivyokuwa vikiwapuliza wateja taratibu ili warejee tena siku nyingine. Mako si mtu wa starehe, ila huhudhuria maeneo haya mara chache sana. Mwenyewe hudai, hutembelea kule, ili kujifunza dunia inakwendaje.
Kiota kile cha burudani, kilijaa watu, lakini hawakuwa wengi kiasi cha kukosa nafasi na kuchukiza. Baadhi ya watu walicheza kila wimbo uliopigwa na ‘dj’ ambaye muda wote mikono yake haikutulia kwa sababu ya kuchanganya nyimbo za kukonga nyoyo za wateja. Mako hakucheza, alikaa akipata kinywaji chenye kilevi.
Akiendelea kusukuma mafunda kadhaa ya kinywaji chake, alimwona binti mrembo akiingia ndani ya kiota kile cha burudani. Nishai zilishamkaa sawasawa, akapaza sauti, “mrembo, njoo ukae katika kiti.” ni kama bahati, kwani binti yule hakupinga, alitembea kwa madaha kama twiga mbugani kisha akaketi pembezoni mwa Mako!
“Unaitwa nani mrembo?” Mako aliuliza.
“Lightness.”
“Jina zuri sana, mimi pia ninalo jina, ninaitwa Mako.”
Mazungumzo yao yalifana, hata ungewaona ungedhani walifahamiana kitambo. Walizungumza, wakacheka na wakati mwingine walinyanyuka wakacheza mziki pamoja.

Bofya Hapa Kujiunga Kundi la Riwaya za Mwalimu Makoba WhatsApp
Mako alidhani labda binti yule ni kahaba kwa sababu ni kawaida kwa wanawake wa aina hiyo kuingia katika viota vya starehe. Hata hivyo, alishangazwa na jinsi binti huyo alivyokuwa. Hakuwa na tabia za mabinti wanaojiuza. Miongoni mwa sifa yao kuu, ukicheza nao ni lazima waombe bia. Hali ilikuwa tofauti, Lightness alinunua kinywaji chake mwenyewe. Hapo Mako akaanza kubaini kabisa aliyekuwa naye hakuwa kahaba bali ni binti mpenda burudani tu.
“Unaishi wapi?” Mako aliuliza.
“Mtaa wa Mwanaukome.” binti alijibu, safari hii kazidi kulegea sababu ya kile kinywaji.
“Unaishi na nani?”
“Ma mkubwa!”
“Kakuruhusu kuja huku?”
“Nimetoroka!”
Maswali yalimwishia Mako, ikabaki kucheza mziki na kunywa kinywaji. Mako aliwaza kimoyomoyo, “leo pesa yangu haijaenda bure!” pengine ni kwa sababu ya mauno aliyokatiwa na binti Lightness, binti huyu ni kama hakuwa na mfupa katika kiuno chake, Mako akafaidi, wengine wakalitoa jicho wakila kwa macho.
Lakini ghafla burudani ikakatishwa baada ya mlio wa risasi kusikika, watu wakataharuki wanaotaka kukimbia.
“Wote lala chini… wote lala chini.” waliamrisha vijana wawili ambao walivaa kofia zilizoficha sura zao.
Watu walitii amri, walilala chini kama mizoga, hata Mako na Lightness walilala chini.
Itaendelea Jumapili...

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu