Jinsi ya Kuandika Kumbukumbu za Kikao| Mfano kutoka NECTA

Jinsi ya Kuandika Kumbukumbu za Kikao| Mfano Toka NECTA

Nikiwa nimekaa katika kiti kikubwa cha kuzunguka, mbele nikitazama ugomvi wa buibui na siafu, siafu alionekana kuelemewa kiasi kifo kilimwita kwa sauti ya upole.
“Mwalimu, kuna tatizo,” nilishtushwa na sauti ya mwanafunzi.
“Tatizo gani?” niliuliza.
“Mwalimu wa waalimu, sijui kuandika kumbukumbu za kikao, swali hili laweza toka  kwenye mtihani nikakosa alama.”
“Usiwaze alama pekee, katika maisha halisi, unaweza kushindwa kuandika kumbukumbu za kikao kinachokuhusu endapo utapewa jukumu hilo. Kuna baadhi ya nchi usipoweza kuandika kumbukumbu za kikao unafungwa jela!” nilimaliza kwa utani, wote tukacheka, kisha msafara wa watu wawili kuelekea darasani ukafuatia.

Jinsi ya Kuandika Kumbukumbu za Kikao

Unapoandika kumbukumbu za kikao, hakikisha unazingatia mambo manne ambayo ndiyo sehemu ya kumbukumbu za kikao:
1. Kichwa cha habari
2. Waliohudhuria
3. Wasiohudhuria
4. Ajenda
Ajenda imegawanyika katika mambo manne:
I. Kufungua kikao
II. Maandalizi
III. Mengineyo
IV. Kufunga kikao

Sasa tutazame mfano kutoka swali la necta mwaka 2011.

Andika kumbukumbu za kikao cha wanafunzi kuhusu sherehe ya kumuaga mkuu wenu wa shule aliyepata wadhifa wa kuwa Afisa Elimu wa Mkoa.
MUHTASARI WA KIKAO CHA KAMATI YA WANAFUNZI KUANDAA SHEREHE YA KUMUAGA MKUU WA SHULE KILICHOFANYIKA 24/06/2011 KATIKA UKUMBI WA SHULE KUANZIA SAA 5.00 ASUBUHI MPAKA 7.00 MCHANA.
A. WALIOHUDHURIA (wawakilishi wa madarasa)
I. Beatrice Ngonyani IA
II. Stella Oswald IIA
III. Mkolosai Emsii IIIB
IV. Ahmed Juma IV B
V. Manwa Kigoma (Mwenyekiti)
VI. Rashid Abubakar (Katibu)
B. WASIOHUDHURIA
I. BALQIS KOROFI (bila taarifa)
II. LUJJAYNA MWEUPE (kasafiri)
C. AJENDA
I. Kufungua kikao
II. Maandalizi
III. Mengineyo
IV. Kufunga kikao

I. Kufungua kikao

Mwenyekiti alifungua kikao mnamo saa tano kwa kuwakaribisha wajumbe na kuwaomba wawe huru kuchangia katika kikao hicho.

II. Maandalizi

Ili kufanikisha sherehe hiyo, wajumbe waliamua kuchagua kamati ndogo ambayo ingesaidia katika kufanikisha sherehe. Wajumbe wa kamati waliochaguliwa ni:
A. Beatrice Ngonyani IA
B. Stella Oswald IIA
C. Mkolosai Emsii IIIB
D. Ahmed Juma IV B

III. Mengineyo

Wajumbe walikubaliana kuchangia kiasi cha shilingi 1,000/= ili kumnunulia zawadi mkuu wa shule. Pia, walikubaliana kuhamasisha watu wajitokeze kwa wingi katika sherehe ya kumuaga mkuu wa shule.

IV. Kufunga kikao

Mwenyekiti alifunga kikao kwa kuwaomba wajumbe wawafikishie taarifa wanafunzi wote kuhusu yaliyokubaliwa katika kikao na kutoa ushirikiano ili kufanikisha sherehe. Kikao kilifungwa saa 7.00 mchana.
….……………………                                 …………………………….
Manwa Kigoma (Mwenyekiti)                     Rashid Abubakar (katibu)
Tarehe 24/06/2011                                     Tarehe 24/06/2011

Popular posts from this blog

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne