Wanasiasa Wanahama Mchana Kweupe, Hata Aibu Hawaoni| Makala za Mwalimu
Ni ujinga kama tutafurahia kufa
kwa upinzani! Nchi isiyo na watu wenye mawazo tofauti, inasikitisha na kutia
simanzi! Ole wetu Watanzania.
Kipindi hiki kimekuwa na
purukushani za wanasiasa kuvihama vyama vyao kwa wingi zaidi kuliko katika
kipindi chochote ambacho nimekuwa nikizifuatilia siasa za Tanzania. Katika hama
hama hii, wengi wanadai yale waliyokuwa wanayataka yafanywe, sasa yanafanywa na
Chama Tawala hivyo hawana sababu ya kuendelea kuwa wapinzani. Hoja hii ni
dhaifu na ina walakini. Kwani uhai wa upinzani upo pale tu chama tawala
kinapofanya madudu? Kama hali ni hii, basi hatujui maana na lengo la vyama
vingi.
Hata hivyo, ukweli huwa
haujifichi. Sababu moja katika nyingi inayowafanya wanasiasa hawa wahame kutoka
huku kwenda kule (chama tawala kwenda upinzani na upinzani kwenda chama tawala)
ni ‘maslahi binafsi’. Hapa kuna makundi mawili yanaibuka:
Kundi la kwanza ni lile la
wanasiasa wasio na kitu. Hawa hawana mali. Ni masikini ambao wameamua iwe
iwavyo lazima watumie umaarufu wao wa kisiasa kujitengenezea kipato ili
kupambana na ugumu wa maisha. Hawa wako wengi kuliko aina nyingine yoyote ile.
Kundi la pili ni la wanasiasa
wenye kitu. Hawa wana mali nyingi sana. Ni matajiri wanaonesa katika mabembea!
Kinachowasumbua hawa ni hofu tu. hofu ya kushuka, hofu ya kufilisika. Hawana
amani kuwa katika vyama vyao, suluhisho la kulinda mali ni kusarenda na kusema,
‘tumerudi bwana mkubwa! Tusamehe sana!
Wote hawa si wazuri kuwakabidhi
madaraka. Watu wasio na misimamo ni hatari kwa afya ya taifa. Ni watu
wanaovutwa na upepo wa fedha, hawana uwezo wa kutafakari sentimita chache mbele
ya matumbo yao laini. Wanaisaka shibe, na bila shaka wameipata.
Ugumu wa maisha umetengeneza
wimbi kubwa la wanasiasa wasio na upande maalumu. Hawa ni watu ambao wanatumia
nguvu kubwa kujifanya wakosoaji wa mambo katika nchi ili waonekane. Wakiisha
kuonekana, wanaweka dau mezani wanunuliwe! Inachosha.