Sitasahau Nilipolala na Mwanamke Juu ya Kaburi (27)| Riwaya
Nilishtuka nikaamka. Shingo
iliuma lakini nilijikaza. Nilikuwa mahali nisipopafahamu, nazo fahamu zikazidi
kunirejea taratibu hata nikagundua palikuwa pangoni.
“Umetumwa kuja kuniokoa! Lakini
nimekudondosha kwa kofi moja tu.” Mtoto alizungumza, bila shaka ni Chimota.
“Sijabobea katika ulozi!”
nilijibu.
“Nani kabobea?”
“Wewe, inasemekana ulizaliwa
nao.”
“Ulishuhudia wakati nazaliwa?”
“Hapana. Niliambiwa tu.”
“Ujinga ni kukubali kila
unachoambiwa!” alinijibu. Nikakaa kimya.
Nilizungumza na Chimota mpaka
tukazoeana. Nilipomuuliza aliwezaje kuishi pangoni badala ya kuishi katika
falme ya Matumbawe, alinijibu kuwa, aliutoroka utawala huo baada ya kugundua
walitaka kumtumia katika mambo ya kunyanyasa watu wengine. Pia aligundua siri
kuwa, yeye hakuwa mzaliwa wa Matumbawe, bali aliibwa kichawi na kufikishwa
huko. Alipogundua nguvu zake za ziada, hakusita kukimbia. Hata hivyo, hakujua
hasa ni kwa namna gani angerudi tena nyumbani, ujio wangu mahali pale ulimpa
faraja na matumaini makubwa.
Sikutaka kuuliza aliwezaje
kunitambua, jibu nilikuwa nalo. Yote yalisababishwa na ulozi. Baada ya muda nilimwona
akiwa amelala, nikalala pembeni yake.
Ilikuwa asubuhi tulivu
iliyonikuta nikiwa ndani ya pango kama nungunungu. Ajabu ni kwamba, ndege
hawakuimba. Palikuwa kimya hata pakaogofya. Mwenyeji wangu hakuwako! Nilishtuka
nikatoka ndani haraka. Nilimkuta akiwa nje. Kakaa chini anasoma kitabu
nisichokifahamu.
“Chimota,” niliita.
“Mimi hapa,” aliitika.
“Nashukuru nimekupata, naomba
tuondoke muda huu tuanze safari ya kurejea nyumbani. Nitajitahidi kubahatisha
njia. Hatuwezi kupotea, Samike atasaidia.”
Chimota alinitazama kwa udadisi
kisha akaachia tabasamu jembamba. Alionekana kuafiki maneno yangu. Niliinama
kumwondoa mdudu mdogo aliyekwama katika mguu wangu wa kulia. Nilipoinuka
sikumwona Chimota! Niligeuka nyuma tayari kuanza kumtafuta. Sikuamini nilichokiona!
Askari niliowakimbia msituni
wakiongozwa na yule mtu wa kitengo cha kunusa walizikamata vyema silaha zao za
jadi. Walikuwa wengi kiasi cha kushindwa kuwaza chochote. Nilipatikana mzima
mzima na ujanja wangu wote sasa ulibaki mfukoni.
Nilifungwa kamba ngumu mikononi
kisha nikaamrishwa nitembee mbele. Nilitii maagizo nikaongoza njia hata
nikafanana na mtumwa anayepelekwa uhamishoni wa kosa la kukataa amri ya bwana
wake.
Tulitembea mpaka tulipofika
katika lango la kuingilia mjini. Bila shaka lilikuwa lango la kuingia ndani ya
utawala wa nchi ya Matumbwe. Tulipoingia, watu walipanga mistari pembezoni mwa
njia na wote walinizomea kwa hasira.
Kila nilipokuwa napita, yule
askari mwenye pua kubwa aliwaambia watu kuwa, mimi ndiye chanzo cha mvua
kutonyesha. Wengi walikasirika, baadhi yao wakanirushia mawe. Hata hivyo,
hayakunipata.
Niliendelea kutembea pembezoni
mwa umati mkubwa wa watu huku nikizushiwa kashifa mbalimbali zisizothibitika
kisayansi. Mwisho niliingizwa katika kasri la mfalme. Nikiwa humo, nilipelekwa
mpaka katika chumba kikubwa kilichokuwa bora sana. Kwa jinsi nilivyotekwa,
nilistaajabu kuingizwa katika chumba safi kama kile. Kilikuwa kikubwa,
pembezoni paliwekwa kitanda murua na godoro, viti vinne vilivyopakwa dhahabu
viliizunguka meza ndogo iliyong’aa. Niliona mlango mmoja pembezoni mwa chumba,
humo palijengwa bafu la kifahari! Nilifikiri labda watakuwa wamekosea kuniweka
mule na punde wangekuja kuniondoa na kunipeleka chumba cha mateso
nilichostahili.
Itaendelea Jumanne…
“Si ruhusa kuchukua hadithi hii na kuiweka katika mfumo wa sauti, kutoa kitabu, kuweka katika blogu au ‘website’ nyingine, au kufanya chochote kile bila kuwasiliana na mmiliki! Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka!”
Daud Makoba 0754 89 53 21