Riwaya| Sitasahau Nilipolala na Mwanamke Juu ya Kaburi (25)
Haikuwa kama nilivyofikiri.
Majoka yale hayakuniwinda mie, bali yaligombana yenyewe kwa visasi vya muda
mrefu. Nilikaa chini sehemu ambayo isingekuwa rahisi kudondokewa na viumbe hivi
hatari.
Majoka yalipigana yakaumizana
vibaya. Yaliunguzana mbavu kwa ule uwezo wake wa kutema moto. Mwisho yote
yalikuwa hoi, kwa pamoja yakadondoka kwa kishindo, “Puuuuh!”
Niliachana na mkasa ule
nikaendelea na safari yangu. Sikumwona tena yule ndege. Nikabaki mpweke
msituni.
Wakati nikiendelea kutembea, niliona
kikapu kikiwa kimetundikwa juu ya mti. Nilisogea haraka mwenye shauku ya kujua
kilichokuwa kikapuni. Nilifika nikasogeza mkono niweze kukigusa. Sikufanikiwa. Kumbe
ulikuwa mtego, ulifyatuka ukanifunga kamba miguuni na kunining’iniza kichwa
chini miguu juu. Mimi na kikapu wote tukaelea juu kwa juu.
Hali ya kuning’inizwa namna ile
ilikera na yalikuwa mateso makubwa.
Nilikwisha choka kutembea, mkasa wa kuning’inizwa kama nyama buchani ulinikata
maini. Nikachoka tena na tena!
Baada ya muda mrefu, nilisikia vishindo
vikija niliponing’inia. Niliogopa kiasi. Hatimaye walinifikia watu ambao
walivaa ngozi ambazo hata hivyo zilitumika kufunika sehemu nyeti pekee. Mwili
mwingine ukaachwa upate raha na karaha ya jua.
Walionekana kuwa wawindaji
mashuhuri katika msitu ule. Nao wakanisogelea, waliponiona, walinitazama kwa
hasira. Nilitambua sababu ya hasira yao. Mtego waliotegemea kupata nyama,
alinasa mwanadamu asiyeliwa! Niliwaharibia hesabu zao.
Mmoja wao alizungumza kwa hasira,
“We nyau katika umbo la mtu! Ndiyo nini kunasa wakati mtego haukuhusu… jamii
yetu inakufa njaa leo siku ya tatu hatujapata chakula kisha unaharibu mtego…
umetumwa na Hissopo?”
Aliyezungumza alitaja jina jipya
ambalo sikulifahamu. Nadhani watu hawa walikuwa na uhasama mkubwa sana na
Hissopo. Nilitamani kujua lakini sikuwa na taarifa. Nikiendelea kushangaa, nilimwona
yule mzungumzaji akizungumza na wenzake. Sikugundua mapema alichowaeleza.
Baadaye niliwaona wote wakitikisa
vichwa vyao. Kumbe Mzungumzaji aliwashawishi wanile mimi ili kupunguza makali
ya njaa ambayo punde ingeiteketeza jamii yao.
Basi nilibebwa mzobemzobe
nikaanza kupelekwa nisipopajua. Walinipeleka huku wakiimba nyimbo zisizovutia
hivyo haikuwa na maana kuzikumbuka.
Tulitembea mpaka tukafika katika
kijiji kilichojengwa nyumba za nyasi. Lango la kuingilia kijijini lilikuwa
wazi, lakini badala waingie, walikunja kona, tukaanza kutembea pembezoni mwa
ukuta. Nilisimama kuona kilichokuwa ndani ya ukuta ule. Kilikuwa kijiji kizuri
sana, lakini watu wake, walikonda vibaya. Niliweza kuhesabu mbavu za ajuza
mmoja.
Niligundua kilichowasumbua watu
hawa, njaa kali. Hata hivyo sikuwa tayari kugeuzwa kitoweo kuwaokoa.
“Wewe uliyenasa kwenye mtego
usiokuhusu nisikilize kwa makini!” alisema Mzungumzaji, “sisi si watu wabaya,
ila njaa imetufunza ukatili. Hatujakuingiza kijijini kwa sababu maalumu, jamii
yetu haili watu. Hivyo ili watu wasikatae kula nyama yako, tumeamua kukuchinja
pembezoni mwa ukuta wa kijiji. Tukuchune, kisha tuwapelekee nyama yako. Tazama
jiwe lile mbele yako, utachinjwa pale!”
Itaendelea Jumapili…
Tunaomba radhi kwa simulizi hii
kutoruka Jumapili hii kama ilivyokawaida. Tunajitahidi kuhakikisha jambo hili
halijirudii tena.
“Si ruhusa kuchukua hadithi hii na kuiweka katika mfumo wa sauti, kutoa kitabu, kuweka katika blogu au ‘website’ nyingine, au kufanya chochote kile bila kuwasiliana na mmiliki! Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka!”
Daud Makoba 0754 89 53 21