RIWAYA| SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (22)

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (22)

KAMA ULIIKOSA SEHEMU ILIYOPITA ISOME HAPA: SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (21)
Kisha endelea kuisoma...
Mzee Samike alikuwa uvunguni. Nilistaajabu nikauliza, “umefikaje nami nimekuacha nje?” hakunijibu. Alicheka akitoka chini ya uvungu na kukaa kitandani.
“Unafahamu kisa cha mimi kupelekwa jela?” aliniuliza.
“Sifahamu mzee…”
“Nilimfanyia mauzauza afisa mmoja wa jeshi la polisi. Kwa hasira akanitengenezea kesi bandia. Hata hivyo hawakuniweka sana wakaniachia!”
“Ndiyo mzee… nilikuona gerezani nikiwa katika harakati za kukutafuta!”
“Hata mimi nilikuona!” Alijibu, tukabaki tukitazamana kwa mshangao!
“Chakula chako kiko sebuleni… kwa sasa nahitaji kuzungumza nawe kuhusu kuyakomesha haya mauzauza yako,” mzee alisema. Nikapata matumaini.
Tulifanya mazungumzo yaliyonipa matumaini makubwa. Mzee alinambia amekwisha mzuia mtu wa ajabu na kamwe sitamuona tena. Nilifurahi nikashangilia kwa ushindi. Pia, mzee alisema hapendi kuniona nikihangaika na kazi zisizoeleweka, akaniomba nihamie kwake ili nishirikiane naye katika shughuli ya uvuvi. Sikuwa na pingamizi, nilikubali mwenye furaha ya kutosha. Nikiwa na matumaini ya kufanikiwa na kudhani mwisho wangu wa kupambana na vitu vya ajabu ulifika, jambo jipya likaongezeka.

“Asante kwa kukubali kuishi hapa na kushirikiana nami katika shughuli za uvuvi,” mzee alishukuru, “hata hivyo, kuna kazi naomba unisaidie!”
“Kazi gani tena mzee? Uvuvi ndo huu… kuna kingine?” nilihoji.
“Ndiyo… mjukuu wangu Chimota hakufa kama unavyodhani!”
“Tobaaah!” nilishtuka.
“Amini… mimi nilizaliwa na ulozi wangu mkononi. Wachawi wote walinifuata kunitaka nijiingize katika uchawi wao na wanga. Nilikataa kufanya uchawi wa kuwadhuru watu, sikukubali… sikuwa tayari kumkamata mwanadamu mwenzangu nimfanya msukule… nilipinga jambo hilo.
“Basi wanajumuiya wenzangu wakaniona msaliti kwao, wakafanya hila za kila namna. Wakanichonganisha na wanajamii wote wanaonifahamu hata nikakosa rafiki. Watu wote wakaniogopa kuwa mimi ni mtu hatari ninayesababisha misiba ya watoto wao… kuogopwa huku ndiko kumenifanya leo hii niishi katika jumba hili la upweke.
“Walipoona wamenichonganisha na kunikosesha amani kwa kila kitu, ndipo walipoamua kuniharibia familia yangu pekee niliyoishi nayo kwa furaha. Walimchukua binti yangu mapema sana baada ya kujifungua. Walimtia uzuzu, akapambana nao kisu kwa kisu, wakaona wakimwacha atawamaliza wakamwua na kumtupa katika bonde la hasara.

“Binti yangu aliniachia kijukuu kizuri cha kiume… jina lake Chimota. Alilala hapo ulipolala wewe, nilipenda alivyoota. Ndoto zake zilijaa matumaini. Kuna kipindi aliota chuki kati ya watawala na watawaliwa imekwisha nayo roho ya kisasi imemezwa na kumeng’enywa. Kuna wakati aliniacha hoi alipoota ati vijana wote wenye nguvu kawaona wamepata kazi, hakuna hata mmoja anayekaba na kufanya uzinzi kama uliofanya wewe Mako.
“Wachawi hawakufurahishwa na hikima iliyojaa katika kichwa cha mjukuu wangu Chimota. Wakambeba. Watu wote hudhani Chimota alikufa… la hasha! Chimota yungali hai katika nchi ya matumbawe. Kavundikwa na hawaishi kutaka kumbadili awe na akili kama zao. Awe katili kama wao. Hawataweza!” mzee alimaliza, nami nikauliza swali:
“Bila shaka unahitaji msaada wa kumrejesha mjukuu wako, lakini mimi si mlozi. Huoni kama watanipiga kwa pigo moja tu mzinzi mimi?”
“Asante kwa kunielewa… ishi na mimi, nitakufua vyema na hakuna atakayeweza kupambana na wewe! Chimota atarudi. Nawe utamrejesha!
Tulimaliza mazungumzo yale na mzee. Nikamwomba ruhusa nifuate vitu vyangu ili nihamie kabisa mahali pale. Mzee hakusita, aliniruhusu nami nikatumia masaa matatu kukamilisha shughuli ya uhamishaji wa vifaa vya kapuku.
Asubuhi sana, mimi na mzee tuliongozana kuelekea baharini. Mzee alivalia kaptura ya kijivu na shati jeupe lililochoka kiasi. Mimi nilikuwa na suruali nyeusi na fulana ambayo kusema kweli siitambui rangi yake kwa sababu ya ule mpauko ilioupata baada ya kuwekwa mwilini kwa miongo kadhaa. Basi mimi na mzee tukatembea haraka kuiwahi safari ya kuvua samaki.

Tulifika baharini mzee akafungua nanga ya mtumbwi wake na pasipo kupoteza muda, mtumbwi ukaivamia bahari na kuisabahi kwa salamu ya kuwataka samaki wa maji chumvi.
“Mzee sasa tumezama chumvini!” nilitania. Mzee akacheka!
Mtumbwi ulisogea taratibu hata tukafika mbali. Lakini ghafla mimi na mzee tuliliona wimbi kubwa likija. Nikapatwa na mshituko mkubwa nisiyejua cha kufanya.
Itaendelea Jumapili…
“Si ruhusa kuchukua hadithi hii na kuiweka katika mfumo wa sauti, kutoa kitabu, kuweka katika blogu au ‘website’ nyingine, au kufanya chochote kile bila kuwasiliana na mmiliki! Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka!”
Daud Makoba 0754 89 53 21
Shusha maoni yako mdau!...

TAZAMA POVU LA MWALIMU MAKOBA KWA WASANII WAVAA HOVYO

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Sifa Bainifu za Irabu ya Kiswahili Sanifu