KALIO LA JIRANI YANGU LILIVYOZUA BALAA
Dunia ina mambo na vijimambo nami
nashukuru nimefanikiwa kushuhudia vituko vingi mno maishani mwangu. Ni majuzi
tu hapa nimeshuhudia kisanga cha aina yake baada ya kalio la jirani yangu kuzua
balaa.
Jina lake aliitwa Sakina. Ni
jirani yangu kwani kwangu na kwake wala si mbali. Kama walivyo waswahili
wengine, naye hajawahi kuweka wazi umri wake. Hata hivyo, kwetu sisi wenye
jicho la tatu, tuna uhakika lazima atakuwa na miaka 26.
Alijaaliwa sura nzuri sana na
rangi ya maji ya kunde, nywele zake zilikuwa habari nyingine, hakuhitaji kuvaa
wigi jirani yangu huyo. Japo alikuwa mzuri katika kila idara, alikosa kitu
kimoja, hakuwa na kalio kabisa. Yaani huko nyuma palikuwa ‘flat’ kama chapati
vile. Basi jambo hilo lilimkosesha raha. Vijana wa mtaani waliomtongoza akawakatalia
walimuumiza zaidi walipomwambia, “mwanamke mwenyewe tako huna… una ringa nini?”
Baada ya muda jirani yangu Sakina
alipotea hata tukaogopa kwa kudhani labda alitekwa na watu wasiojulikana. Kumbe
alikwenda sehemu kutafuta suluhisho la matatizo yake. Alihitaji kuongeza kalio
lake, hivyo akampata rafiki mmoja aliyempeleka kwa mtaalamu ambaye alimpatia
dawa za kichina tayari kabisa kwa kuyajaza maumbile ya nyuma!
Basi bwana, baada ya miezi
kadhaa, Sakina akarejea akiwa kafungasha kwelikweli, kalio lilijaa vyema na
kutengeneza shepu ambayo sijawahi kuiona kokote mie!
Kwa kuwa watu walimcheka ‘hana
kalio’, akaamua kuuonyesha mtaa mzima kuwa, masikini kapata matako na sasa
anayaliza mbwata!
Alikodi ngoma kwa lengo la kupita
mtaa mzima kuonyesha umbile lake hilo la kununua.
Akiwa na vijana wapiga ngoma na
tarumbeta aliowakodi, alianza kupita kila sehemu akitikisa kalio ili watu
waone! Alimaliza chochoro zote akiwatambia watu kuwa sasa yuko juu na ametimia
kwa kila kitu. Hatimaye sasa akafika katika kijiwe nilichokaa mimi na masela
kibao ambao mpaka leo hatuna ajira japo tuna degree kubwa kubwa kutoka vyuo
vinavyoeleweka.
“Semeni tena sina tako, oooh
mwanamke mkia huna unaringa nini?” Sakina alisema akitutazama, wapiga ngoma
wake wakashangilia, “Oyoooooooh!”
Alipoona hatuna cha kujibu ila
tunamtolea macho tu, akaanza kuzungusha kiuno chake kama mnenguaji wa bendi,
watu wake wakashangilia, sisi tukabaki tukitoa macho na kujiramba kwa sinema ya
bure! Alipomaliza kukata mauno, akaanza kutikisa makalio. Likitikisika hili,
linafuata lile hata ikawa kama gari inawasha ‘indiketa’.
Alizidisha visa alipoona watu
wanamshangilia. Sasa akaanza kurukaruka juu. Kila aliporuka kalio lilinesa
isivyokawaida, watu wakashangilia, sisi tukatoa macho na kujiramba. Aliruka
kalio likanesa! Akaruka tena kalio likanesa zaidi, aliporuka mara ya tatu,
oooooh… salaleeeeeeh! Kalio likapasuka kwa kishindo kikubwa, “pwaaaaah!” Sakina
akadondoka chini akiwa kapoteza fahamu!
Kwa sasa tumegawana majukumu. Sisi
tumembeba jirani yetu Sakina tunampeleka hospitali, na wale wapiga ngoma wake,
tumewaacha wanavikusanya vile vipande vya kalio la kichina.
#Makoba