Siri ya Utupu

SIRI YA UTUPU
UTUPU ni hali ya kutokuwa na kitu. Huenda ukawa utupu wa pochi, chumba, mali, akili na hata utupu wa mwili. Wahenga wa zamani (sio hawa wa mitandaoni), waliupuuza utupu kwa kusema, Mkono mtupu haurambwi.
Hali ya utupu hivi sasa inazidi kubadilika kwa kasi. Utupu umegeuka kitu. Utupu unategemewa kumvusha mtu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Tazama nyimbo za wanamuziki zilivyo. Wasichana wanaotumika humo  wanacheza utupu kabisa. Hawaogopi lolote na hata aibu hawaoni.
Zamani wazee walipotaka kumwaga laana, walitishia kuwaonesha watoto wakorofi utupu. Enzi hizo kuonekana kwa utupu ilikuwa ni laana kubwa. Wapo ambao walichanganyikiwa na kuwa wehu kwa sababu ya kadhia hii.
Vibinti vya dhama hizi vinapiga picha za utupu bila kuogopa chochote. Ukiviuliza kwa nini vinafanya hivyo, utasikia vinajibu kuwa vinapenda kuwa hivyo… vinapenda kukaa utupu. Ujinga mtupu.
Hali ya mabinti kukaa utupu kwa kiasi kikubwa imepunguza hamu ya vijana kuoa. Ndio, vijana wanaona kila kitu. Sasa aoe ili aone nini kingine.
Maadili yamebadilika sana sasa. Ni kweli kuwa hapo zamani mwanadamu alitembea utupu. Lakini tamaduni hubadilika kulingana na wakati. Mwanadamu tangu kupata ustaarabu wake, utupu si jambo la kuonesha hadharani.
Bado ninaendelea kutafakari nguvu hii ya utupu kukamata hisia za watu imetoka wapi? Ni kweli wanaowachezesha mabinti wakiwa watupu namna ile watafurahi wakiwaona watoto wa kuwazaa wao wakifanya vile? Lazima sasa turejee katika maadili. Heshima iwepo.
Jamaa mmoja aliwahi kunieleza kuwa, utupu kuzidi kuonekana mara kwa mara kumemwaga laaana kali katika jamii. Ndiyo maana kila kukicha limeibuka lile, mara limetokea hili.
Sina uhakika kama kuna sheria inayoeleza lolote kuhusu mavazi. Ni wakati wa kulitafakari hili kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Ni utupu wa fikra kuamini kuwa utupu unaweza kukupatia mafanikio. Sana utaambulia, kupata umaarufu wa mpito.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu