Sarakasi za Makinikia: Wasomi Waliweka Elimu Mfukoni
Wasomi wengi katika nchi za kiafrika
linapokuja suala la kusaini mikataba inayogusa rasilimali za taifa, huwekeza
nguvu nyingi katika vidole huku vichwa vikiachwa vifanye kazi ya kubeba bongo
tupu!
Inashangaza kusema kuwa, walioliingizia
hasara taifa hili katika sakata la MAKINIKIA ni watanzania ambao kwa idadi yao
hawazidi watano… wasomi, waliobeba bongo tupu, AKILI NDOGO ZINAZOENDESHWA NA
TUMBO!
Makampuni ya wakala wa meli ya Freight Forwarders
(T) Limited, Quick Services Clearing and Forwarding Limited na Walford Meadows
Co. Ltd, ziliwasilisha nyaraka za uwongo za usafirishaji wa makinikia kutoka
Kahama Mining Corporation, (baadaye Bulyanhulu Gold Mine Ltd) na Pangea Minerals
Ltd, katika kipindi cha kati ya mwaka 1998 na 2017. Kwa miaka 19 wasomi wetu
walikuwa wakidanganywa, nasi tukiwalipa kodi zetu watutumikie. UCHURO!
Katika maandiko yangu yaliyopita niliwahi
kushauri kwamba, tusiwafundishe watoto wetu historia ya sayansi, bali
tuwafundishe sayansi yenyewe! Ni ajabu wasomi wetu waliamini kwamba kilichokuwa
kikisafirishwa ni mchanga mtupu, kana kwamba wazungu wale walikwenda
kutengenezea matofali. Ukweli ni huu, mchanga uliouzwa nje ya nchi haukuwa
mchanga hasa badala yake, yalikuwa ni madini ya aina mbali mbali mahususi
yaliyopatikana kutokana na uchenjuaji kwa njia ya ‘carbon–inleach’ (CIL).
MTANZANIA ALIYEFUNDISHWA HISTORIA YA SAYANSI BADALA YA SAYANSI HAWEZI AKAUJUA
MFUMO HUU SIKU ZOTE ZA MAISHA YAKE.
Madini mengi kama dhahabu, Silver, Copper, Sulphur, Iron, Nickel, Zinc
na Madini yote ya kundi la Platinum ambayo yalisafirishwa kwa
kivuli cha mchanga, kama pesa yake ingekwenda
serikalini, serikali ingeweza kuajiri waalimu wote wa sanaa na sayansi
na kuachana na porojo rojorojo kuwa waalimu wamejaa. Pia serikali ingeweza
kutoa mikopo kwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu hata wanaosoma mapishi wangepata
100%. Katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia, serikali ingeweza kuununua
mtandao wa WhatsApp, facebook, twitter na instagram. AMINI MANENO YANGU,
NAZUNGUMZIA DOLA ZA KIMAREKANI BILIONI 144.77 sawa na trilioni 380.499, pesa
hiyo ikiandikwa kwa tarakimu asilimia 99 ya watanzania hawataweza kuisoma, 380,499,453,421,688.