SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya 12)

hawakukataa walitukumbatia kisha wakatutakia kila la heri katika safari tuliyotaraji kuianza. Kabla hatujaondoka nilikifuata kile kijitu ambacho kiliiba mwezi wetu na kuzungumza nacho maneno ya mwisho.
          “Mwezi wenu utakapozima, usiwaze kuja kuiba mwezi wetu, chukua kitabu hiki kinatoa maelekezo ya jinsi ya kuuwasha mwezi uliozima.” Nilisema huku nikikikabidhi nakala moja ya kitabu.
Mimi na Minza tulipanda Mapandagila, nikamweleza Minza kuwa mimi ndiye ningekiendesha chombo kwa wakati huu ili nami nipate uzoefu wa kuongoza chombo kilichosifika pande zote za Dunia.
Tulipaa mpaka ulipokuwa mwezi wetu, mwezi ukaongeza tabasamu, Minza akachomoa kamba kubwa iliyokuwa na sumaku maalumu ya kuunasia mwezi, mwezi ukanasa katika kamba, nasi tukapaa, sisi mbele, mwezi nyuma tukiuvuta kama mkia. Furaha yetu haikuelezeka kwa wakati huo.

Baada ya masaa mengi ya kupaa angani, hatimaye tulifika katika eneo ambalo vichawi vya anga viliwahi kunishambulia, mapigo yangu ya moyo yakaanza kwenda mbio, Minza akanituliza na kunieleza kuwa mapatano ya amani yalikwisha fanyika kati ya vichawi vya anga na nchi yetu. Tena akaongeza kuwa nchi yetu haikuwa na adui hata mmoja. Nilifurahishwa na habari hizo nikaichochea Mapandagila.
Tulifika Duniani saa mbili usiku, Dunia ilitawaliwa na giza kali ambalo hata almasi isingeweza kuonekana. Lakini ghafla kwa sababu ya ule mwezi tuliouvuta nyuma ya Mapandagila yetu, mwanga wa kutosha uliimulika Dunia, nilichungulia chini, mamilioni ya watu walishangilia kupatikana kwa mwezi. Masikini wengi wao walidhoofika kwa sababu ya madhara ya kukaa bila mwezi, sasa tulirejesha matumaini.
Tulifika mahala unapokaa mwezi, Minza akaondoa ile kamba iliyoufunga, ukabaki huru, safari hii haukuishia kutabasamu tu, mwezi ulicheka na kila ulipocheka mwanga uliongezeka.
Tuliuacha mwezi na kutua chini ya ardhi yetu tuipendayo, ardhi ya nyumbani, ardhi ya mababu zetu ambayo tuliithamini na hatukuwa tayari kuishi kokote. Tulipokelewa kishujaa na watu wote, wenye vyeo na wasiokuwa na vyeo. Nilimuona ndugu yangu Mowasha akishangilia kwa furaha, lakini kwa bahati mbaya sikukumbuka kumletea zeze kutoka nchi ya vijitu kama alivyoniagiza, nilipanga maneno mengine ya kumridhisha. Mfalme alikuwepo katika mapokezi, alijivunia kuwa na taifa lenye watoto imara na wenye maarifa ya kurejesha chochote kwa maslahi ya nchi yao.
Tulichukuliwa na kikosi maalumu kwa heshima zote mpaka kwenye gari dogo la kifahari, safari ya kuelekea Ikulu ikaanza. Kufumba na kufumbua tulifika ikulu, mimi nikapewa chumba changu, Minza binti mfalme akaenda katika chumba chake cha siku zote. Wafanyakazi sabini na watano walioajiliwa kuhudumu katika chumba changu walinitaka nilale kwa sababu ya uchovu wa ile safari ya mafanikio ya kuusaka mwezi.
Nililala kwa furaha nikisubiri kukuche ili mimi na Minza tufanyiwe sherehe kubwa ya kihistoria katika ardhi ya Lahaja.
                                                     
                                                MWISHO
Jumapili ijayo itaruka riwaya mpya ya kusisimua, MCHEZO WA JOGOO.
USIKOSE...
Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu