RIWAYA| SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya 11)
“Kama mnayosema ni
kweli niko tayari kuwapatia mwezi wenu.” Alijibu mfalme.
“Tunakushukuru sana kwa kukubali,
tunaomba mambo yote haya tuyakamilishe kesho asubuhi ili tuweze kurejea
nyumbani… wazee wetu wanateseka.” Alimalizia Minza, ukawa mwisho wa mazungumzo
yetu na mfalme.
Asubuhi ilikuwa
tulivu, tayari mimi na Minza tulikwisha amka na tulikuwa tukisubiri ruhusa ya
kupaa kwenda kuutengeneza mwezi wao na kuuchukua mwezi wetu.
Kikosi maalumu
kiliandaliwa kwenda na sisi, walipewa agizo moja tu, kutuua endapo tungeshindwa
kuuwasha mwezi wao. Pia walielezwa endapo mwezi wao ungewaka basi waturuhusu
kuondoka na mwezi wetu hukohuko angani.
Sekunde chache kabla
hatujaondoka Minza alimfuata mfalme akanong’ona naye jambo, hapana shaka
alimweleza, “Hatutauawa tunaouwezo wa kuuwasha mwezi wowote, kokote na muda
wowote!”
Sisi tulipanda katika
Mapandagila yetu, askari wengi wa vijitu waliokuwa zaidi ya elfu moja
wakatusindikiza, wao wakipaa kwa miili yao, nasi tukipaa kwa Mapandagila.
Minza ndiye
aliyekiongoza chombo, mimi niliendelea kukisoma kitabu kilichoeleza namna ya
kuuwasha mwezi uliozima. Baada ya mwendo wa masaa mawili, Minza alipunguza
mwendo nikagundua kuwa tumekaribia kufika, nikakiweka kitabu changu pembeni.
Niliweza kuona miezi
miwili ikiwa imekaribiana, mwezi wao haukutoa mwanga wowote hata ulianza
kubadilika na kuwa mweusi. Mwezi wetu uling’ara kama tochi hata ulipotuona
ukatutambua na kutoa tabasamu pana.
Tulitua katika mwezi
wao, nikafukua chini taratibu kisha nikapigapiga mara kumi, nikagundua kuwa
mwezi wao ulizima kwa sababu walizidisha mafuta wakati wanausafisha. Nilichukua
kifaa kidogo katika Mapandagila yetu, Minza akanisaidia kubeba baruti ndogo,
tukashirikiana kukizika kile kifaa na ile baruti kisha nikawaamuru wote wasogee
mbali kiasi. Baada ya dakika tano, baruti ile ililipuka na kile kifaa
nilichoweka kikapaa juu kisha kikarudi kwa kasi na kuzama chini umbali ambao
hatukuutambua, mara ghafla mwezi wao ukawaka na kutoa mwangaza tena. Wote
wakashangilia kwa furaha.
Wakiwa na furaha,
nilisogea karibu yao kwa unyenyekevu mkubwa, nikaweka mikono yangu kifuani
kisha nikawaomba waturuhusu tuondoke na
mwezi wetu,
Itaendelea jumapili…