‘ACT’ WAZARENDO NI ‘CCM’ KIBUBUSA?

bendera ya ACT inapepea mlingotini
Kibubusa ni kufanya jambo bila ya kujulikana, yaani kisirisiri. Wazarendo hawa kama wajiitavyo, wamekuwa wakizua maswali mengi kila kuchapo kama ni kweli hawa nao ni wapinzani au ni maigizo na ngonjera zisizokwisha?
Kumbukumbu zinaeleza wazi kwamba, aliyekuwa injini ya maarifa ya chama hicho, Profesa Kitila mwana wa Mkumbo alipatiwa cheo serikalini akihusika na sekta ya maji ambayo hata hivyo toka aingie hakuna mabadiliko yaliyofanyika labda ahadi. Hata hivyo kama wasemavyo wanasiasa, tumpe muda, atatimiza.
Hivi punde, aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho, Mama Anna Mgwira, anatangazwa kumrithi Meck Sadick katika nafasi ya ukuu wa mkoa wa Kilimanjaro. MGHWIRA KAULA!
Maswali mengi yanaibuka hapa, mosi, kama wapinzani wanapewa vyeo kwa lengo la kuonesha ukomavu wa kisiasa, kwa nini ni ACT peke yao ndio wanaodondokewa na neema hii ilhali kuna vyama vya upinzani zaidi ya 20 hapa nchini?
Pili, kama utoaji wa vyeo hivi unalengo la kuua upinzani, ACT wanakipi cha kutisha hata wauliwe? Kwa nini mbinu hii isitumike kuua CHADEMA, CUF na jamaa zao wa UKAWA?
ACT wanakazi nzito ya kuwaaminisha watu kuwa wao sio CCM B. Kwa vyovyote vile, si jambo la kawaida kwa serikali kumkabidhi mkoa mpinzani makini, kwani kufanya hivyo ni kupunguza nguvu ya ushawishi ya chama chake katika mkoa huo. Sababu hii imepelekea kwa miaka dahari, ukuu wa mikoa kupewa makada wa kufa na kupona bila kujali uwezo wao wa kuchakata mambo ilimradi tu wanajua kusoma na kuandika.
‘ACT’ WAZARENDO NI ‘CCM’ KIBUBUSA? Swali hili linaweza kujibiwa na kitu kimoja tu…
WAKATI.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie