SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya tisa)


“Panda haraka tuondoke!” Minza alisema kwa sauti kubwa. Nikatembea haraka mpaka ndani ya Mapandagila nikaingia ndani nikakaa katika kiti kimojawapo kati ya viti viwili vilivyokuwamo.

            “Hii Mapandagila inao uwezo wa kubeba watu wawili?” nilimuuliza Minza.

            “Hii inaouwezo marambili zaidi ya ile uliyokuja nayo.” Alijibu Minza kisha akairusha juu Mapandagila, huku akituma taarifa makao makuu, “Mapandagila itakimbia mwendo wa sauti kumi na nane za kunguru dume.” Kisha haoo tukapotelea angani na kuiacha nchi ile ya watu wa chuma.

            “Naweza kuendesha sasa? Naona mfumo wake sawasawa na Mapandagila zilizopita… tofauti ndogo tu, nitazimudu.” Nilimuomba Minza.

            “Hapana… umechoka sana na akili yako haijatulia, wacha niendelee utaendesha wakati tukiurejesha mwezi nyumbani endapo tutaupata.”

            “Sio endapo tutaupata, ni lazima tutaupata na kuurejesha ukiwa salama salmini.” Nilifoka. Minza akanyamaza. Chombo kikayakata mawingu.

Tulitembea kwa kasi kwa muda wa masaa mengi nisiyoyakumbuka. Ghafla mbele yetu tukaona kitu kikubwa kikielea angani. Ilikuwa sayari ya Vumu, mioyo ikaturipuka kwa furaha.
Minza aliongeza kasi ya chombo chetu, chombo kikatikisika, kwa mwendo kiliokuwa nao, hata mwanga usingeweza kutupata. “Vuum.” Tuliingia katika sayari ya Vumu, tukakaribishwa na joto kali. Nilifurahi sana kuingia katika nchi ya viumbe wa ajabu, raia wa Vumu ni watu pekee ambao waliweza kupaa bila mabawa, walipoamua kukimbia walikimbia bila kuchoka tena kwa kasi zaidi ya gari moshi.


Minza akapunguza kasi ya chombo, huku tukiwaza ni wapi palikuwa sehemu sahihi kutua. Lakini tukiendelea kuwaza, askari wa Vumu waliokuwa doria angani, walituona, tulishangaa kuona watu waliopaa bila kutumia mabawa, wakazungumza nasi kwa sauti za kutisha.

Itaendelea jumapili...

Nachukua nafasi hii kuwapa pole wazazi na watanzania wote kwa kuondokewa na wanafunzi, wapendwa wetu, katika ajali ya Karatu. mwenyezi Mungu azipumzishe mahali pema roho za marehemu wote. Comment Amen.

Daud Makoba.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2023

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne