RIWAYA| SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya 10)“Jitambulisheni nyie ni akina nani? Sivyo tunawachoma moto.” Alisema mmoja wao aliyeonekana kuwa kiongozi.
          “Tumekuja kwa amani,” nilijibu, “sisi ni wanadamu toka sayari ya Dunia, tupelekeni kwa mfalme wenu tuna mazungumzo.”
          “Ha! ha! ha! mmeufuata mwezi wenu, hampati kitu, na mkileta habari za kudai mwezi mtarudi bila roho zenu.” Kilijibu kijitu kichafu, nilipokitazama usoni nikagundua ni kilekile kilichoiba mwezi wetu na kuuweka mfukoni, nilistaajabu umbile dogo la kiumbe yule liliwezaje kuubeba mwezi tena kwa kuutia mfukoni!
Baada ya mazungumzo walikubali kutupeleka kwa mfalme wao. Walitutaka twende kwa mwendo pole ili tufike asubuhi maana usiku ule mfalme alilala na haikupaswa kumsumbua.
Chombo kilitembea taratibu tukiwa tumewekwa katikati ya vile vijitu, hatukuruhusiwa kuongea wala kukohoa. Kwa muda wote huu, msichana Minza hakuonesha dalili yoyote ya kuchoka wala hofu.
Wakati kunakucha, sisi tulikuwa tunaingia katika makazi ya mfalme wa Vumu. Sayari hii ilitawaliwa na mfalme mmoja, na watu wake wote walifanana. Walikuwa wafupi, wachafu, lakini wanaoweza kupaa.
Tulipofika chombo chetu kilitua, nikashuka na Minza akashuka, tukapelekwa mpaka ndani, humo tulimkuta mfalme akiwa amekaa katika kiti cha dhahabu. Mfalme hakufanana na watu wake. Alikuwa mrefu tena asiyeweza kupaa, msafi na mwenye nywele za sufi tofauti na watu wake ambao wote vichwa vyao havikuwa na nywele. Mfalme alitukaribisha nasi hatukusita, tulikaa katika viti.
          “Habari ya Duniani?”
          “Nzuri.” Tulijibu kwa pamoja.
          “Endapo mmekuja kuchukua mwezi wenu hamtafanikiwa, na endapo mmekuja kutembea karibuni sana.” Mfalme alizungumza maneno ambayo yalitukatisha tamaa hata kabla hatujapumzika. Kauli hiyo ilikifanya kifua cha Minza kidunde kama mpira. Nikaamua kuzungumza kwa busara sana.
          “Ni kweli tunautaka mwezi, lakini hii ni kwa faida yetu sote. Sisi na wewe. Mwezi wa Dunia yetu ulitengenezwa kwa ajili ya Dunia yetu, kuuweka huku kunaufanya utoe mwanga hafifu na kikifika kipindi cha kupatwa kwa jua mwezi huu utasababisha majanga ya asili. Zipo faida mbili za wewe kuturuhusu kuondoka salama na mwezi wetu.”
          “Zitaje.” Alijibu mfalme akiwa na hamu ya kufahamu. Nikamtazama machoni Minza aliyekuwa kimya muda wote kisha nikaendelea kuzungumza.
          “Tunafahamu ya kwamba nyinyi si viumbe waovu ila mmeiba mwezi wetu kwa sababu mwezi wenu ulizima ghafla. Hivyo tutauwasha tena mwezi wenu na kuwafundisha namna ya kuutengeneza pindi uharibikapo.”
Mfalme aliachia tabasamu pana hata nikaweza kuyaona meno yake meupe. Akatulia kwa muda akitafakari.

Itaendelea Jumapili...

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Tamthiliya ya Kilio Chetu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024