KISA CHA DEREVA WA GUTA KUZAMA KISIMANI
Guta ni baiskeli yenye mataili
matatu, lakini Bwana Sakasaka hataki kabisa guta lake kuitwa baiskeli, yeye
analiita SCANIA. Jana aliitwa na Mama Kidomo ambembee vyombo vyake kwa sababu
alikuwa anahamia mtaa wa saba kwa kuchoka chokochoko za majirani.
Vyombo vyote vya ndani ikiwemo
kabati, kitanda, na masofa vilienea katika guta! Basi Bwana Sakasaka
akaingia barabarani na guta lake likiwa limejaa mzigo. Alipoikamata barabara
kuu, alikutana na foleni kubwa akaamua kuivamia barabara ya waenda kwa miguu.
Waenda kwa miguu walikuwa wengi, lakini hakujali, akalichochea guta lake
likakolea mwendo kwelikweli. Hakuwa na kengele, alisikika akiwaonya waenda kwa
miguu, “Tahadhari, SCANIA hii, ikikugonga hunyanyuki!”.
Basi akiendelea na mwendo. Mara ghafla mbele yake, alitokea mtoto mdogo
akikimbia, dereva wa guta akavuta breki lakini haikushika. Akakunja kona ya
ghafla, ghuta hilo likatumbukia kisimani! “Chumbwiiiii.”
Kwa sasa tupo hapa tumemrushia kamba
ili atoke, lakini akina mama wa mtaani wanalalamika. “Katuchafulia maji mshenzi
huyu! Katuchafulia maji mshenzi huyu!”