JAZA UJAZWE! UPEMBA MWINGI NA TAFSIRI ZA KIMOMBASA
Lugha
ya Kiswahili ina maneno lukuki ambayo kama hutakuwa makini katika uchaguzi
utaibua sintafahamu na mishangao kwa watu! Hata kabla ya ‘jaza ujazwe,’ neno ‘tigo’
peke yake lina maana nyingine mbali na maana yake!
Ama
hakika, muhusika wa kitengo cha matangazo kutoka kampuni ya ‘tigo’ atakuwa
amefanikiwa sana kuitangaza biashara na ofa hii mpya ya kampuni yake. Lakini mbali
na faida hiyo, kuna ukakasi mkubwa ambao umetanda miongoni mwa watu hasa wanaotambaa
na maana ya ziada. Wengi hususani wanaume, wanaona neno hili si zuri kutumika
na linawadharirisha.
Makampuni
ya simu yamekuwa na tabia ya kuigana kila inapotokea kampuni mojawapo ikaja na
ubunifu wa kuvutia. Lakini katika hili makampuni pinzani bado yako kimya,
hakuna aliyejibu mashambulizi haya. Kinacholeta ugumu ni kupata maneno yasiyo
na ukakasi. Jekejeke litatokea endapo makampuni mengine yatakuja na misemo hii:
CHOMEKA UCHOMEKWE, TIA UTIWE, WEKA UWEKWE, NYONYA UNYONYWE, GEUZA UGEUZWE,
LAINISHA ULAINISHWE na mengine mengi ya aina hiyo.
Ukiangalia
kwa undani maneno haya hayana maana mbaya, ila kwa kuwa maana katika lugha huwa
ni zaidi ya ile maana ya msingi, ukakasi kama huu ni lazima kutokea.
Lugha
kuwa na utata na kuibua maana nyingi ni kiashiria kwamba imekua. Hili ni pigo
kwa wanaodhani bado tunapaswa kuendelea kufundisha maarifa kwa lugha ya
kiingereza. Kwa miaka dahari na dahari, kiswahili kimekuwa na msamiati wa
kutosha. Nafunga pazia hapa, kama umependa waraka huu wa dharura, basi MINYA
UMINYWE!