SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya saba).
Nilikaa ndani ya chumba kile mpaka nilipopitiwa na
usingizi, nikiwa usingizini niliota jinsi watu wa nchi yangu walivyokuwa
wakiteseka, kabla ndoto haijaisha niliamshwa na binti waziri, mkononi
akanipatia mikate miwili iliyotengenezwa kwa ufuta, nikagundua upembe ndio
ulileta chakula hicho.
Nilikula mikate ile mpaka nikaimaliza, wakati
nikiendelea kuusikilizia utamu wa mkate, binti waziri alinishika mkono kisha
akasema nami taratibu.
“Hakuna
aliyewahi kukataa agizo la mfalme, kesho asubuhi utaondoka kwenda kuvichukua
vitabu vya mafanikio… usiogope, utasindikizwa na askari kadhaa.”
“Siwezi
kwenda, watu wangu wanateseka.” Nilibisha, binti akatoka ndani na kuufunga
mlango. Nikabaki katika chumba nikiwa mpweke.
Nikiwa ndani ya chumba kile, niliwaza mengi, kubwa
zaidi nilifikiri namna ya kutoroka ili niendelee na safari yangu. Ulinzi
ulikuwa mkali nilipata hofu kiasi.
Nilikitazama chumba chote, sikuweza kuona upenyo, kwa
huzuni nikapitiwa usingizi. Nilistushwa usingizini na ukelele hafifu
niliousikia… nilipotazama mbele kidogo niliona sakafu inanyanyuka juu, kisha
akaibuka mwana mfalme, Chokusi. Kumbe ndani ya chumba kile palikuwapo handaki!
Chokusi alisogea karibu yangu akanikumbatia,
nikafarijika kwani nilipata uhakika kuwa alikuja kunisaidia.
“Rafiki yangu umekula?” aliniuliza.
“Ndiyo.”
“Kesho asubuhi wanapanga kuondoka na wewe, wametumwa
askari zaidi kutoka matawi yote waje wahakikishe kuwa hutoroki, nafasi pekee
uliyonayo ni sasa. Ukichelewa kidogo tu, hutapata upenyo tena.”
“Nisaidie rafiki yangu…” niliomba kwa sauti ya
unyonge.
“Nipo hapa kwa ajili hiyo… haya haraka tuingie katika
shimo hili tutembee mpaka tutakapoibuka upande wa pili.”
Chokusi alitangulia, mimi nilifuata, tukazama ndani ya
shimo kama nyoka, tukatembea kwa tahadhari kubwa ya kukamatwa na askari. Moyoni
nilianza kupata furaha ya kuendelea na safari yangu.
Tulitembea kwa mwendo mrefu mpaka tulipoibuka mahali
ambapo sikupafahamu, nilifurahi lakini nilikumbuka jambo moja nikaamua kuuliza.
“Asante
sana… lakini nadhani hapa ni mbali sana, na Mapandagila tumeiacha nyumbani.”
“Mapandagila?
Kile chombo chako cha kuelea angani?... Tazama pale mbele”
itaendelea jumapili...