SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya nne)

Tukiwa njiani kuelekea katika mji wa jitu hili, nilijitahidi kuuliza maswali.

            “unaonekana u mtu mwema kwangu lakini watu wa jamii yako hawatanidhuru?”

            “hakuna awezaye kukugusa!”

            “kwa nini?”

            “mimi ni mwana wa mfalme.”

Nilifurahishwa na jibu hili na lilinipatia furaha, wakati tunaendelea kutembea tuliufikia mji na niliona nyumba zilizojengwa na watu hawa wa chuma. Nyumba zao zilijengwa kwa vioo vigumu na zilifanana sana hata haikuwa rahisi kubaini wapi aliishi tajiri na wapi aliishi maskini.

Wakati tukiendelea kutembea majitu mengi yaliendelea kunikodolea macho na kunishangaa sana, lakini hawakuthubutu kunigusa nilikuwa na mwana mfalme.

Punde tulifika katika jumba kubwa, jumba lilikuwa tofauti na nyumba nyingine, jumba hili lilijengwa kwa dhahabu pekee. Hapo hapo nikagundua nilikuwa ndani ya nyumba ya kifalme. Mwenyeji wangu aliiweka Mapandagila 214 katika uwanja wa jumba lile.

Tuliingia ndani, mbele kidogo nikamuona mfalme, mfalme akacheka kisha akasema,
            “Chokusi, leo umeleta kiumbe dhaifu kutoka sayari ya Dunia!!”

Hapo nikagundua kuwa mwana mfalme aliitwa Chokusi, nilipomtazama usoni alicheka, kisha akanambia nisiogope hakuna baya litakalonipata.

            “Kiumbe toka Duniani jitambulishe.” Mfalme alitamka.

            “Naitwa Nkenye, nipo katika safari ya kuusaka mwezi ulioibwa na kijitu toka Vumu.” Nilijibu.

Mfalme alicheka kisha akaniambia,

            “Wanadamu ni viumbe wa ajabu sana, mtoto mdogo kama wewe kupewa kazi ya kuutafuta mwezi ni unyanyasaji.”

Sikutaka kumjibu mfalme, kuna mambo ambayo hakuyafahamu, nilikaa kimya.

Tulizungumza mengi na mfalme na alidai ya kuwa wao wanajua uwepo wa wanadamu waliotengenezwa kwa nyama lakini sisi hatujui uwepo wao watu wa chuma. Kikubwa zaidi mfalme aliahidi kunisaidia kufika katika sayari ya Vumu.

Mwana mfalme alinichukua na kunipeleka uwanjani, wakati tunaelekea huko niligundua kuwa viumbe hai vyote katika sayari hii viliumbwa kwa chuma. Nilistaajabu nilipokutana na mbwa wa chuma, akataka kunirukia, rafiki yangu Chokusi akamkata kofi zito, mbwa akafyata mkia na kukimbia.


Niligundua kuwa kumbe mwanamfalme pamoja na urefu wake wa futi sita na nguvu alizokuwa nazo, alikuwa na umri sawa na wangu, yaani miaka tisa!

Itaendelea jumapili.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne