MSIMLAUMU ANTHONY JOSHUA, AMEFANYA KAZI NILIYOMTUMA

Haina ubishi tena kuwa Anthony Joshua ndiye mfalme wa ndondi katika zama zetu. Laiti kama angeishi katika zama za akina Mohammed Alli, George Foreman, na Joe Frazier historia ingebadilika kidogo. Kizazi cha akina Tyson, Evander na Lenox Lewis hakimuwezi, mwakilishi wao Klitchko kapigwa vilivyo.
Pambano lake la leo, limefunika pambano la wale vijana wa uzito wa manyoya, Mayweather na mwenzake Pacquiao… ngumi zimepigwa mpaka kivumbi kikatimuka.
Kabla pambano halijaanza, nilipata kumtumia ujumbe kijana wangu Anthony Joshua uliosomeka, “its not over untill its over”, Joshua hakusita kuujibu kwa kusema, “Next Stop The Ring.” Kisha akazima data.
Pambano la Klitchko na Joshua lilipoanza, round ya kwanza mpaka ya tano, Joshua alishambulia sana kwa mapigo yote ya kifundi. Watu walimshangilia kama kawaida, huku mimi nikitafuta namna nzuri ya yeye kushinda.
Ilipofika Round ya sita, Joshua alionekana kuchoka kidogo hii ni kwa sababu kwa round tano mfululizo alikuwa akirusha makonde, basi mpinzani wake kutoka urusi, akaitumia nafasi hiyo. Klitchko alirusha jeb kali, ikampata Anthony, wakati bado hajatafakari Klichko akaongeza right hook kali sana ambayo ilimdondosha chini Anthony. Ukumbi wote ukakaa kimya, watu wakajua tayari Klitchko kashinda, naye Klitchko, akajiandaa kushangilia ushindi. Wakati Anthony akiwa chini akiugulia maumivu ya ngumi mbili nzito, ndipo akayakumbuka maneno yangu niliyomwambia kabla ya pambano, “Its not over untill its over.” Kijana akajikaza kiume, akainuka ili aendelee kupambana, akafuta jasho katika bega lake la kulia ambalo amelichora ramani ya Afrika. Akaanza tena kurusha ngumi.
Katika raundi ya kumi na moja, Joshua aliamua kumaliza mchezo, alirusha jeb kali, ikaupiga uso wa Klitchko, akapiga jeb tena, mara right hook, jeb, right hook, jeb, upper cut, jeb, right… oooh salalee Klitchko huyo, kadondoka chini. Lakini Klitchko naye si wa mchezo, akajizoazoa na kusimama. Khe! ni kama aliuchokonoa mzinga wa nyuki… alipokea ngumi kali mfululizo zilizomfanya amung’unyemung’unye maneno. Mara huyoo chali kifo cha mende. Joshua kamaliza kazi niliyomtuma.  USHINDI!
#Makoba

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika Risala | Kiswahili Kidato Cha Nne