SAFARI YA KUUSAKA MWEZI (sehemu ya pili)
Hatutaki uhasama wala vita tena katika nchi hii… hivyo
atakayekwenda huko aende kutatua matatizo kwa njia ya Amani.” Mfalme alikohoa
kidogo kisha akaendele kuzungumza kwa sauti kubwa zaidi,
“Kama
mjuavyo chombo chetu cha masafa ya mbali huwa hakiwezi kupandwa na mtu mzima
ila mtoto mdogo tu kwa sababu ya nguvu ya mvutano ya Dunia, hivyo anatakiwa
apatikane mtoto mdogo asiyezidi miaka 15 na asiyepungua miaka minane…”
Kabla mfalme hajaendelea kuzungumza, nilipaaza sauti
huku nikisogea mahala aliposimama,
“Mimi
Nkenye, nitakwenda Vumu kuusaka mwezi, nina umri wa miaka tisa, nimekuwa
nikifanya kazi ya kuusafisha mwezi pale unapochafuka na kutoa mwanga hafifu,
pia mimi ni mtoto wa shujaa Mako aliyemwangamiza mfalme wa vichawi vya anga kwa
kipande cha sindano butu!”
Umati mzima ulinishangilia, mfalme akanikumbatia, bila
shaka ni kwa sababu ya ujasiri mkubwa niliouonesha. Watu wote waliamuliwa
kuondoka, baba, mama na kaka yangu Mowasha walibaki kunitakia kwa heri ya
kuonana! Baba alinisogelea na kuninong’oneza maneno haya,
“Wewe
ni mtoto wa shujaa nenda kaipiganie nchi yako… usitetereke!” nilitikisa kichwa
kuashiria kwamba nilikubaliana na maneno yake, kisha aliniachia, mama
alinifuata akanikumbatia, hakusema neno, Mowasha alinishika mkono huku akisema,
“Ukifika
huko, nichukulie zeze… nasikia vijitu ni vitaalamu vya kutengeneza vyombo vya
muziki!”
“Ha!
Ha! Ha! Nitakuletea…” nilijibu, baada ya hapo mkuu wa usalama akanichukua,
ndugu zangu wakaelekea nyumbani.
Mkuu wa usalama alinipeleka mpaka katika chumba
maalumu ambacho kiliandaliwa kwa ajili ya kuniaga, humo ndani alikuwamo mfalme
na mawaziri wake wote, nilipofika
niliwasalimu kwa heshima kisha nikakaa katika kiti kimojawapo. Mfalme
alisimama akaanza kuzungumza.
“Nkenye,
jambo hili ni la haraka sana hivyo hatuna muda wa kupoteza, tumekuita humu
kukuaga na kukutakia kila lenye heri katika safari yako, utaondoka sasa hivi
kwenda kuusaka mwezi, utapaa na chombo cha Mapandagila214… wewe si mgeni katika
kutumia chombo cha masafa ya mbali hivyo tunategemea mafanikio makubwa kutoka
kwako.” Mfalme alimaliza, wote wakanipigia makofi kama ishara ya kunitia moyo.
Mfalme na watu wengine wote waliokuwamo waliinuka,
wakanipeleka katika uwanja mpana uliokuwa katikati ya jengo la mfalme ambapo
hapo ndipo Mapandagila 214 ilihifadhiwa. Mapandagila 214, ilifanana na jabali
gumu, ilikuwa kubwa kutosha kukaa mtoto mmoja tu. Kilikuwako chombo kingine cha
masafa ya mbali kiliitwa Mapandagila 107. Hiki kiliacha kutumika baada ya
kuvumbuliwa Mapandagila 214 ambacho kilikuwa cha kisasa zaidi.
Tulifika na kumkuta binti mfalme aliyeitwa Minza
akimalizia kuifuta Vumbi Mapandagila 214. Minza alikuwa na umri sawa na wangu,
binti huyu alipenda sana kufanya kazi hata ungemwona usingedhani kwamba alikuwa binti mfalme!
Itaendelea Jumapili...