Sarufi ya Kiswahili | Kiswahili Kidato cha Tano Mada ya 1

Wanafunzi wakiwa darasani wanasoma sarufi
Sarufi ni kanuni zinazoongoza matumizi ya lugha.

Dhana za fonimu na alofoni za lugha ya Kiswahili

Dhana za fonimu na alofoni hujitokeza katika tawi la sarufi matamshi. Vilevile, tawi hilo huitwa fonolojia.

Fonolojia ni tawi la sarufi linalohusika na uchunguzi na uchanganuzi wa mfumo wa sauti za lugha mahususi.

Mfumo wa sauti za lugha hujengwa na vipashio mbalimbali.

Kipashio cha msingi katika fonolojia hujulikana kama fonimu.

Fonimu ni sauti zote za lugha zenye uwezo wa kupambanua au kutofautisha maana katika maneno ya lugha fulani mahususi.

Fonimu za lugha zimegawanyika katika makundi mbalimbali ambayo ni:

- Konsonanti

- Irabu

- Viyeyusho

Fonimu hutofautiana kwa idadi kutoka lugha moja hadi nyingine.

Mathalani, Kiswahili kina jumla ya fonimu thelathini zilizogawanyika katika makundi yaliyotajwa.

Katika Kiswahili, kuna irabu tano ambazo ni: /i/, /ɛ/, /u/, /ɔ/, /a/;

Konsonanti ishirini na tano ambazo ambazo ni /p, b, t, d, k, g, f, v, θ, s, z, ʃ, ʒ, tʃ, dʒ, h, m, n, ɲ, ŋ, l, r, j, w/;

na viyeyusho viwili ambavyo ni /w/, na /j/. Hapa, fonimu hizo zimeandikwa kwa alfabeti ya kifonetiki.

Fonimu hubainishwa katika makundi mbalimbali kwa kuzingatia sifa zake za utamkaji. Sifa hizi huitwa sifa bainifu. Sifa hizo hutokana na mahali sauti inapotamkiwa, namna inavyotamkwa na hali ya nyuzisauti wakati wa kuitamka.

Kutokana na namna fonimu zinavyotamkwa, tunapata sauti za:

Vipasuo /p, b, t, d, k, g/,

sauti za vikwaruzi /f, v, s, z, θ, ð, ʃ, h, x/,

sauti za vipasuo-kwamizi /tʃ, dʒ/,

sauti za viyeyusho /j, w/,

sauti za ving’ongo au nazali /n, m, ŋ, ɲ/,

sauti ya kimadende /r/

sauti ya kitambaza /l/.

Kutokana na mahali pa matamshi, tunapata sauti za:

Midomo /p, b, m, w/,

sauti za ufizi /t, d, s, z, r, l, n/,

sauti za meno /θ, ð/,

sauti za midomo-meno /f, v/,

sauti za kaakaa gumu /tʃ, ʃ, j, ɲ/,

sauti za kaakaa laini /k, g, ŋ, y/,

na sauti ya glota /h/.

Kutokana na hali ya nyuzisauti, tunapata sauti:

ghuna /b, d, g, v, z, ð, ʒ, j, z, m, n, ɲ, ŋ, l, r/

na sauti zisizo ghuna ambazo ni /p, t, k, f, s, θ, ʃ, h/.

Irabu zote ni sauti ghuna.

Kwa hiyo, sifa bainifu za sauti, mathalani /t/ ni kipasuo, ufizi, si ghuna.

Irabu zina sifa bainifu zinazotokana na:

Mwinuko wa ulimi kutoka chini kuelekea juu,

sehemu ya ulimi inayoinuka

na mkao wa midomo wakati wa kuzitamka.

Kutokana na mwinuko wa ulimi, kuna irabu ya:

chini /a/; irabu za juu /i, u/ na irabu za kati /e, o/.

Kutokana na mahali pa kutamkwa, kuna irabu za:

mbele /i, e/,

irabu ya kati /a/,

na irabu za nyuma /u, o/.

Kwa kigezo cha mkao wa midomo, kuna irabu:

viringo /u, o/ na irabu si viringo /i, e, a/ ambazo hutamkwa midomo ikiwa imejiviringa au imesambaa, mtawalia.

Aidha, fonimu moja inaweza kujitokeza kwa namna mbalimbali katika maneno fulani kutokana na mazingira ya ujitokezaji wa fonimu hiyo.

Alofoni ni fonimu mbili au zaidi zenye maana moja. Kwa mfano, matamshi ya maneno nguo, ndoo, na mboga ni /ŋguo/, /ndoo/ na /mboga/. Hivyo, sauti /n/, /n̪/, na /m/ ni alofoni za fonimu moja ambayo ni /n/.

Sababu ya tofauti za fonimu hizo ni mazingira ya utoekaji wake. Fonimu /n/ imejitokeza kama [n] katika mazingira ambapo imefuatiwa na sauti /g/. Fonimu hiyo imebaki kuwa /n/ katika mazingira ambapo imefuatiwa na sauti /d/. Kadhalika, fonimu /n/ imejitokeza kama /m/ katika mazingira ambapo imefuatiwa na sauti /b/.

Fonimu na alofoni zina uhusiano wa karibu ingawa zina tofauti pia.

Tofauti ya fonimu na alofoni ni kwamba, fonimu inabadilisha maana ya neno ilhali alofoni haibadilishi maana ya neno.

Aidha, alofoni hutokea katika mazingira maalumu, yaani mfuatano wa aina fulani wa sauti ilhali fonimu hutokea mahali pengine popote isipokuwa pale tu inapotokea alofoni. Hivyo, fonimu na alofoni hukamilishana.

Hata hivyo, fonimu na alofoni zina mwingiliano mkubwa kwani zote ni sauti za kundi moja na huchangia sifa muhimu za kimatamshi.

Zoezi

1. Tamka sauti /b/, /f/, /ʃ/, /g/, /z/, na /h/, kisha andika sifa zake bainifu kulingana na sifa za kimatamshi unazozisikia.

2. Tumia mifano ya maneno ya Kiswahili kubainisha uhusiano wa fonimu na alofoni katika matumizi ya lugha.

Andika maneno yafuatayo kwa unukuzi wa kifonetiki.
(a) ng’ombe
(b) benki
(c) shughuli
(d) thelathini
(e) ngoma
(f) shaghalabaghala
(g) mvi
(h) mvua

Dhana na miundo ya silabi za Kiswahili

Shughuli

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, vikundi vya KI-TEHAMA, chunguza miundo ya silabi za Kiswahili, kisha tamka maarifa uliyo yapata kubainisha miundo ya silabi za data (a) - (f) uliyopewa.

(a) alisoma
(b) labda
(c) kaboba
(d) watakapomshusha
(e) waliyang’anywa
(f) lambwa

Dhana ya silabi

Silabi ni dhana inayoorejelea sauti au fungu la sauti linalotamkwa mara moja na kwa pamoja kama fungu moja la matamshi.

Lugha ya Kiswahili ina silabi:

huru au wazi

na silabi funge.

Silabi wazi au huru ni zile zinazoishia na irabu, kwa mfano, ma- katika neno mama.

Silabi funge ni zile ambazo hutumia sauti za nazali zenye sifa ya kusimama kama silabi kama vile m katika neno mtoto.

Irabu zina uwezo wa kusimama peke yake kama silabi lakini ni silabi huru.

 Miundo ya silabi

Lugha ya Kiswahili ina silabi zenye miundo mbalimbali. Kuna silabi zenye muundo wa irabu pekee (I);

muundo wa konsonanti pekee (K);

muundo wa konsonanti na irabu (KI);

muundo wa konsonanti, kiyeyusho na irabu (KKI);

muundo wa konsonanti, konsonanti na irabu (KKI);

muundo wa konsonanti, konsonanti, kiyeyusho na irabu (KKKI);

na muundo wa konsonanti, konsonanti, konsonanti, na irabu (KKKI).

Muundo

Mfano wa silabi

I

a na u katika neno au

K

m katika neno mti

KI

mi katika neno miti

KkI

kwe katika neno kweli

KKKI

mbwe katika neno mbweu

KKKI

spri katika neno springi

Silabi zenye muundo wa K hujengwa na nazali pekee.

Muundo wa KKKI hutokana na maneno ya mkopo.

Zoezi

1. Chunguza maneno yafuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata:

chungwa

skrubu

mvi

kindumbwendumbwe

mkoloni

(a) Tenga silabi za maneno hayo.

(b) Bainisha muundo wa kila silabi katika maneno hayo.

2. Kwa kutumia mifano kutoka lugha ya Kiswahili, eleza tofauti baina ya silabi funge na silabi huru.

3. Fafanua jinsi miundo ya silabi za maneno ya Kiswahili yaliyokopwa kutoka lugha za kigeni inavyotofautiana na miundo mingine ya silabi za Kiswahili.

Sifa na dhima za viarudhi vya lugha ya Kiswahili katika utamkaji

Dhana ya viarudhi

Viarudhi ni vipengele vya utamkaji vinavyoambatana na vitamkwa wakati wa utamkaji wa tungo za lugha. Viarudhi vinavyopatikana katika Kiswahili pamoja na dhima zake vinafafanuliwa katika vipengele vinavyofuata:

(a) Mkazo

Mkazo ni nguvu inayotumika katika kutamka baadhi ya silabi katika neno.

Kuna lugha zenye mkazo na zisizo na mkazo.

Kiswahili ni lugha yenye mkazo.

Katika lugha zenye mkazo, kuna silabi ambazo zina mkazo msingi (zenye kutumia nguvu kubwa zaidi) na ambazo hazina mkazo msingi.

Mkazo msingi katika lugha ya Kiswahili unaangukia katika silabi ya pili kutoka mwisho mwa neno (silabi ya mwisho kasoro moja).

 Mkazo huu huoneshwa katika kamusi zenye matamshi kwa alama ya ritifaa (') inayopachikwa nyuma au mbele ya silabi inayobeba mkazo huo katika neno.

Katika maandishi ya kawaida, hatuweki mkazo ingawa wasomaji wanajua pa kuweka wanaposoma.

Dhima ya mkazo

- Kufanya utamkaji wa maneno uwe sahihi. Upachikaji wa mkazo katika silabi nyingine yoyote ile huondoa ufasaha.

- Kutofautisha maana za maneno yenye maumbo sawa ambayo maana zake hutofautishwa na mkazo. Hii hutokea katika baadhi ya maneno hususani maneno ya mkopo.

Kwa mfano, sa'limu na 'Salimu, na bara'bara na ba'rabara.

- mkazo hutumika kuonesha msisitizo wa ujumbe ambao msemaji anataka kuufikisha kwa kulitamka neno lenye ujumbe huo kwa mkazo zaidi. Kwa mfano, katika sentensi Nimesema ondoka hapa, msisitizo uko katika neno ondoka na katika Nimesema ondoka hapa, msisitizo uko katika neno hapa.

Ikumbukwe kwamba, ingawa tumeonesha jinsi mkazo unavyowekwa kwenye maandishi, mkazo aghalabu ni kipengele cha kimatamshi.

Kiimbo

Kiimbo ni mpandoshuko wa mawimbisauti wakati wa usemaji.

Kiimbo hubadilikabadilika kulingana na dhamira ya msemaji.

Ikiwa msemaji amekusudia kutoa taarifa au kujibu swali kiimbo kitashuka mwishoni mwa tungo.

Ikiwa atakuwa anauliza swali, kiimbo kitapanda mwishoni mwa tungo.

Aidha, ikiwa msemaji anatoa amri, kiimbo kitashuka au kubaki kati mwishoni mwa tungo.

Kuhusiana na mshangao, kiimbo kitategemea namna mzungumzaji anavyoshangaa; huweza kushuka, kuwa kati, kupanda, kupanda na kushuka au kushuka na kupanda.

Kiimbo husaidia katika kuweka mipaka mikubwa na midogo ndani ya tungo wakati wa usemaji. Mipaka hiyo ni ushukaji na upandaji wa kiimbo katika mipaka ya neno, kirai, kishazi na mwisho wa tungo. Ushukaji na upandaji huu husaidia kuifanya sentensi, hasa ndefu, iweze kutamkika na wakati mwingine, husaidia kutofautisha maana zilizokusudiwa na msemaji.

Tazama, kwa mfano, jinsi tungo zifuatazo zinavyoweza kutatiza maana katika usemaji:

(a) Wanafunzi wenye ufahamu na malengo katika maisha, ambao wana nia ya kufikia malengo hayo, hujituma kusoma kwa bidii, hasa wanapokumbuka kuwa muda wa masomo si mrefu.

(b) A: Baba mdogo mdogo amekuja.      B: Baba mdogomdogo amekuja.

(c) A: Watakao wale ng’ombe wote      B: Watakao, wale ng’ombe wote

Maana ya tungo hizi hutegemea namna mzungumzaji anavyoshusha na kupandisha kiimbo wakati anapozitamka. Hivyo, maana ya tungo huweza kutegemea kulingana na ushushaji au upandanishaji wa kiimbo.

Wakaa 

Wakaa ni muda unaotumika wakati wa kutamka sauti fulani.

Aghalabu, hujitokeza zaidi katika irabu.

Katika taaluma ya fonolojia, wakaa huoneshwa kwa alama maalumu ya nuktapacha (:) ambayo huwekwa mbele ya sauti yenye wakaa mrefu. Sauti yenye wakaa mfupi haiwekewi alama yoyote.

Katika matamshi ya maneno ya lugha ya Kiswahili, wakaa hujitokeza katika namna tofautitofauti.

Katika maneno mengi, wakaa hujitokeza katika irabu za silabi zenye mkazo msingi, kama vile katika neno ana'pi:ma. Hata hivyo, si kila silabi yenye mkazo ina wakaa mrefu; mathalani, neno tobo halina sauti yoyote yenye wakaa mrefu. Kwa hiyo, mzungumzaji anapaswa kuzingatia wakaa sahihi kwa kila neno.

Dhima za wakaa

Wakaa huweza kutumika kutofautisha maana kwa baadhi ya maneno yenye maumbo sawa na maana tofauti, mathalani, majini na ma:jini kama katika sentensi Majini yameingia ma:jini.

Kutofautisha maana katika ngazi ya tungo, mathalani, majibu ya: kitabuni (majibu yamo kitabuni) na majibu ya kitabuni (majibu yanayopatikana katika kitabu).

Zoezi

Soma kwa sauti sentensi zifuatazo, kisha bainisha maana ya kila tungo ukizingatia jinsi zinavyopaswa kutamkwa, hasa katika maneno yaliyolazwa.

(a) Anaona bara'bara.

(b) Anaona ba'rabara.

2. "Mzungumzaji wa Kiswahili anapaswa kuzingatia kiimbo sahihi ili kurahisisha mawasiliano." Thibitisha kauli hii kwa mifano maridhawa.

3. Bainisha maneno matano ya Kiswahili ambayo maana zake zinatofautishwa kwa wakaa, kisha tunga sentensi mbili kwa kila neno.

Dhana za vipashio vinavyojenga neno

Dhana ya mofu

Mofu ni dhana ya kimofolojia inayorejelea umbo dhahiri linaloandikika na kutamkika au lisilodhahiri ambalo linabeba maana ya kileksika au kisarufi. Mathalani, mofu {m-}, katika neno mtoto, inabeba mofimu ya nafsi ya tatu umoja na mofimu ya ngeli ya

Mofu zinaweza kugawanywa katika makundi kwa kuzingatia vigezo viwili:

Kigezo cha maana

Kigezo cha umbo

Kwa kuzingatia kigezo cha maana, kuna mofu huru na mofu tegemezi.

Mofu huru ni mofu zinazoweza kusimama peke yake na kutoa maana inayojitosheleza, mathalani kaka, chupa, ndoo, na maji.

Mofu tegemezi ni mofu zisizoweza kusimama peke yake na kutoa maana inayojitosheleza, mpaka ziungane na mofu nyingine; mathalani, katika neno anapika, mofu a-, -na-, -pik- na -a haziwezi kusimama kila moja peke yake na kutoa maana bila kutegemeana.

Mofu tegemezi ni mzizi wa neno pamoja na viambishi.

Mzizi ni mofu ambayo hubeba maana ya msingi ya neno. Mathalani, -pik- katika neno anapika ndio mzizi.

Kuna aina tatu za mzizi

mzizi sahili

ambatani

huru

Mzizi sahili ni ule ambao hujukaa peke yake bila kuambatana na mwingine kama vile -pik-

mzizi ambatani ni mzizi ulioundwa na mizizi miwili, kama vile -anamwali katika neno mwanamwali.

Mzizi huru ni mzizi unaoweza kusimama kama neno kamili na kutoa maana baada ya kuondolewa viambishi; mathalani, mzizi wa neno anadabiri (a-na-tabiri) ambao ni -tabiri.

Viambishi ni mofu tegemezi zenye uamilifu mbalimbali wa kisarufi ambazo huambikwa au hupachikwa kabla au baada ya mzizi.

Aina za viambishi

viambishi awali

viambishi kati

na viambishi tamati

Hata hivyo, katika lugha ya Kiswahili, kuna viambishi awali na viambishi tamati pekee.

Aina za mofu Kwa kigezo cha umbo

mofu dhahiri

mofu kapa

Mofu dhahiri ni mofu zinazodhihirika kiumbo na kimatamshi.

mofu kapa ni zile ambazo hazina umbo linalodhihirika kimaandishi wala kimatamshi.

Alama inayotumika kuonesha mofu kapa ni Ø kama inavyooneshwa katika mifano wa namba (i) - (iv).

(i) Øjiko → majiko
(ii) Øgari → magari
(iii) Økuta → kuta
(iv) Økucha → kucha

Alama Ø katika mifano (i)-(v) inaonesha kutokuwapo kwa umbo linalobeba mofimu husika katika neno (umoja au wingi), ambayo ndiyo hali ya ukapa.

Dhima ya mofimu

Mofimu ni kipashio kidogo cha kimofolojia kilichomo akilini mwa msemaji wa lugha, ambacho ni cha kinadharia.

Mofimu hubebwa ndani ya mofu.

Mofu moja inaweza kuwa na mofimu zaidi ya moja; mathalani, mofu {a-} katika neno anakula inabeba mofimu ya idadi (umoja) na mofimu nafsi (nafsi ya tatu).

Vilevile, kuna uwezekano wa kuwa na mofimu moja katika mofu mbalimbali, kama ilivyoelezwa katika dhana ya alomofu.

Dhima za mofimu

(a) Kuonesha nafsi na mtenda wa jambo. Kwa mfano:

(i) ninakula - mofu ni- huonesha mofimu ya nafsi ya kwanza umoja.
(ii) anakula - mofu a- huonesha mofimu ya nafsi ya tatu umoja.
(iii) watakula - mofu wa- huonesha mofimu ya nafsi ya tatu wingi.

(b) Kuonesha idadi. Kwa mfano:

(i) m-kulima - mofu m- huonesha mofimu ya umoja.
(ii) wa-lim-sadia - mofu wa- huonesha mofimu ya wingi.

(c) Kuonesha njeo (wakati). Inaweza kuwa wakati uliopo, uliopita au ujao. Kwa mfano:

(i) u-li-lima - mofu li- huonesha mofimu ya wakati uliopita.
(ii) u-na-lima - mofu na- huonesha mofimu ya wakati uliopo.
(iii) u-ta-lima - mofu ta- huonesha mofimu ya wakati ujao.

(d) Kuonesha hali mbalimbali za tendo kama vile hali timilifu, masharti, mazoea na mfuatano wa matukio. Kwa mfano:

(i) Amani a-me-kula.
Mofu -me- huonesha mofimu ya hali timilifu.

(ii) U-ki-ja nitakupa zawadi.
Mofu -ki- huonesha mofimu ya hali ya masharti.

(iii) Mimi hu-anza kazi saa mbili asubuhi.
Mofu hu- huonesha mofimu ya hali ya mazoea.

(iv) Mkurugenzi alikuja, akatoa maagizo kisha akaondoka.
Mofu ka- huonesha mofimu ya hali ya mfuatano wa matukio kwa masimulizi.

(e) Kuonesha urejeshi. Mofu -o-, -ye-, -vyo-, na -zo- zinaonesha mofimu za urejeshi. Kwa mfano:

(i) Wanafunzi wali-o-faulu walipewa zawadi.
(ii) Ng’ombe ali-ye-vunjika mguu yumo zizini.
(iii) Vyombo vili-vyo-nunuliwa ni vizuri sana.
(iv) Nyumba zili-zo-jengwa ni nzuri zinavutia.

(f) Kuonesha kauli mbalimbali za vitenzi kama vile utendeshi, utendea, utendeka, utendwa, utendani na utenda. Tazama mifano ifuatayo kwa kuzingatia mofu ya kauli kama zilivyoorodheshwa:

(i) Waziri Mkuu ameend-esh-a kampeni ya kuchangia damu. (utendeshi)

(ii) Kazimoto alimpik-i-a Subira chakula. (utendea)

(iii) Ardhi hii I-na-lim-ik-a vizuri. (utendeka)

(iv) Mbuzi amechinj-w-a. (utendwa)

(v) Dingiswayo na Zwida wanashauri-an-a. (utendani)

(vi) Mama anapik-a. (utenda, kiambishi tamati -yakinishi)

(vii) Mama hapik-i. (utenda, kiambishi tamati -ukanushi)

Dhana ya alomofu

Alomofu ni maumbo tofauti tofauti ya mofu moja.

Alomofu moja inapotokea, nyingine haiwezi kutokea. Mathalani, katika maneno mw-ili, m-ti, mu-wa, ambazo ni nomino za ngeli ya 1, mofu ya umoja ni {mu-}. Hata hivyo, umbo hilo huweza kujitokeza kama {mu-}, {mw-} na {m-}. Hivyo, ni mofu tofauti tofauti za mofimu moja, yaani alomofu.

Zoezi

1. Fafanua tofauti zilizopo baina ya mofu na mofimu huku ukitoa mifano kutoka lugha ya Kiswahili.

2. Tumia mifano ya Kiswahili kueleza dhana zifuatazo:
(a) mizizi tegemezi
(b) mizizi huru
(c) mizizi ambatani

3. Chunguza data za maneno yafuatayo, kisha bainisha alomofu zinazojitokeza.
(a) mwalimu
(b) muumini
(c) mtu

Vipashio vya neno na dhima zake

Neno hujengwa na mizizi na viambishi, ambavyo hufuatwa viambajengo au vipashio vya neno.

Baadhi ya mizizi katika lugha ya Kiswahili inaweza kusimama peke yake na kutoa maana, kwa mfano, maneno safari, sahau, na baba ni mizizi yenye sifa hiyo.

Mizizi mingine inahitaji viambishi ili neno liweze kukamilika kimaana, kwa mfano, -guu (m-guu/mi-guu), na chez- (chez-a).

Dhima kuu ya mzizi ni kubeba maana ya msingi ya neno, ambayo huwa haibadiliki hata baada ya kuondoa au kubadilisha viambishi.

Viambishi ni mofu tegemezi zinazoambikwa kwenye mzizi wa neno ili kuongeza dhana fulani ya kisarufi au kuunda neno jipya.

Viambishi huainishwa kwa kigezo cha nafasi ambapo vinatokea katika neno.

Katika muundo wa maneno ya Kiswahili, viambishi hupachikwa kabla na baada ya mzizi wa neno.

Aina za viambishi

Viambishi awali

Viambishi vinavyotokea kabla ya mzizi wa neno.

Viambishi tamati

Viambishi vinavyotokea baada ya mzizi wa neno.

Tazama mifano ifuatayo:

(a)
(i) a-na-pik-a
(ii) wa-ta-kimbi-a
(iii) u-me-ruk-a
(iv) ha-tu-ku-m-som-e-a

(b)
(i) a-ta-ni-pig-i-a
(ii) a-me-m-som-esh-a
(iii) m-chez-o

Viambishi vina dhima ya:

kuonesha nafsi

njeo

urejeshi wa mtenda au mtendwa

urejeshi

idadi

wingi

hali

ukanushi

umoja

pamoja na kauli mbalimbali ambazo ni kutenda, kutendwa, kutendeka, kutendana, kutendesha, kutendea na kutendua.

Viambishi hivi hupachikwa katika mizizi kwa njia ya uambishaji.

Uambishaji ni upachikaji wa viambishi katika mzizi ili kuwasilisha uamilifu au dhima mbalimbali.

Kuna uambishaji wa aina mbili

Uambishaji ambatizi

Huu ni uambikaji wa viambishi vyenye kazi za kisarufi.

Uambishaji huu haubadilishi kategoria za maneno kwa sababu unahusisha viambishi vyenye dhima za kisarufi katika neno.

Hii ndiyo sababu inayofanya uambishaji wa aina hii uitwe uambishaji kisarufi.

Viambishi vyenye dhima za kisarufi ni kama vile viambishi vya ngeli, nafsi, njeo, urejeshi, au yambwa.

-pig-

a-na-pig-a

a-na-ye-pig-a

a-na-ye-m-pig-a

Uambishaji nyambulishi (unyambulishaji)

Huu ni uambishaji wenye uamilifu wa kuunda maneno mapya.

Matokeo ya uambishaji huu ni kubadili aina ya neno au kupanua maana ya neno. Tazama mifano ifuatayo:

piga (T) - pigo, kipigo, mpigaji, mpiganaji, pigano (N)

Kauli za vitenzi vya Kiswahili

Kauli za vitenzi vya Kiswahili hubebwa katika viambishi tamati vya vitenzi.

Viambishi hivi huwekwa kabla ya irabu tamati.

Miongoni mwa kauli za vitenzi vya Kiswahili ni:

Kauli ya utenda

Katika kauli hii, kitenzi hubainisha mtendaji wa tendo.

Kitenzi huwa na kiambishi tamati ambacho ni irabu tamati.

Kwa mfano, tukisema, Mwalimu anafundisha, mtenda ni mwalimu na kauli ni ya utenda. Tazama mifano zaidi:

Amani anacheza.

Rehema anaandika.

Ali atalima bustani.

Wanafunzi walifanya mtihani.

Kauli ya utendwa

Hii ni kauli inayoonesha mwathiriwa wa tendo linalotajwa na kitenzi.

Katika kauli hii, mtenda wa jambo si lazima atambulike. Ikiwa italazimika kutambuliwa, basi kitaongezeka kihusishi na kikiambatana na jina la mtenda au kiwakilishi chake.

Mofu ya utendwa ni -w-. Mifano ifuatayo inaonesha kauli ya utendwa katika Kiswahili:

Chakula kimepikwa.

Mwizi amekamatwa.

Nyumba imejengwa na mwashi.

Uchafu umetupwa na mama.

Kauli ya utendeka

Hii ni kauli inayoonesha uwezekano wa jambo kufanyika au kuwa na hali ya kufanyika.

Katika kauli hii, tendo haliwekwi wazi kuwa linatendwa na nani bali huonesha uwezekano wa kutendeka kwa tendo hilo.

Mofu za kauli ya utendeka ni -ek-, -ik-, -lik- na -lek-.

Tazama mifano ifuatayo:

Kitabu kinasomeka.

Kuta zilijengeka.

Wavivu wanafahamika.

Pori linaingilika.

Mazoezi yatafanyika.

Udongo ulizoleka.

Kauli ya utendani

Katika kauli hii, watendaji hufanyiana tendo hilohilo kwa wakati mmoja.

Mofu ya kauli ya utendani ni -an-.

Juma na Paulo watatembeleana.

Watoto wanapeana zawadi.

Mabasi yamepishana vizuri.

Walimu walisaidiana kazi.

(e) Kauli ya utendea

Katika kauli hii, mtendaji hufanya tendo fulani badala, kwa niaba, au kuelekea kwa mhusika mwenyewe. Mofu za kauli hii ni -i-, -e-, -li- na -le-. Tazama mifano ifuatayo:

(i) Mwanahamisi amempikia mtoto chakula.

(ii) Zabibu atamsomea mama yake kitabu.

(iii) Wanafunzi walimkimbilia mwalimu wao.

(iv) Kalimanzila alimzolea bibi yake takataka.

Mofu za kauli ya utendea hujitokeza kama -i- ikiwa mzizi wa kitenzi una irabu a, i au u na huwa -e- ikiwa mzizi una irabu e au o. Ikiwa kitenzi kina irabu a, i au u katika mzizi na kuishia na irabu mbili, basi mofu ya utendea itakuwa -li- na ikiwa mzizi una irabu e au o na kuishia na irabu mbili, basi mofu ya utendea itakuwa -le-.

(f) Kauli ya utendeshi au usababishi Hii ni kauli ambayo inaonesha hali ya kusababisha kutokea kwa tendo fulani. Mofu za kauli hii ni -esh-, -ish-, -z-, -lish-, -lesh-, -fy-, na -vy-. Mifano ifuatayo inaonesha utokeaji wa kauli hii katika Kiswahili:

(i) Bibi alimbebesha mjukuu mzigo wake.

(ii) Pitisha kamba hii kwenye miti.

(iii) Kombo alimwoga bintiye mwezi uliopita.

(iv) Sisi tutamkalisha mtuhumiwa kikao.

(v) Mama amemzolesha Pili uchafu.

(vi) Matukio ya mauaji yanaogofya.

(vii) Sanga alimeza dawa za malaria zikamlevya

Katika kauli hii, kuna maumbo mbalimbali yanayoonesha kauli ya utendeshi. Mofu ya kauli ya utendeshi huwa -ish- ikiwa mzizi wa kitenzi una irabu a, i au u na huwa -esh- ikiwa mzizi una irabu e au o. Ikiwa kitenzi kina irabu a, i au u katika mzizi na kuishia na irabu mbili, basi mofu ya utendeshi itakuwa -lish- na ikiwa mzizi una irabu e au o na kuishia na irabu mbili, basi mofu ya utendeshi itakuwa -lesh-. Vitenzi vingine vichache kama vile lia, lala, jua, toa, na oa hutumia mofu -z-. Vilevile, kuna vitenzi vichache ambavyo hutumia mofu -vy- na -fy-. Kwa mfano, levya katika neno lewa na ogofya katika neno ogopa. Hata hivyo, maneno haya huweza kutumia -sh- kama ilivyo katika maneno lewesha na ogopesha.

Kutokana na mifano hiyo, ni dhahiri kuwa viambishi vya kauli za vitenzi hutokea baada ya mzizi. Viambishi hivi ndivyo huwakilisha kauli mbalimbali za vitenzi katika lugha ya Kiswahili. Aidha, imebainika kuwa viambishi vya kauli moja vinaweza kuwa na maumbo tofautitofauti lakini yakibeba dhana ileile ya kisarufi. Dhana au maana hiyo ya kisarufi huitwa mofimu. Kwa hiyo, maumbo hayo ni mofu tofauti za mofimu moja, yaani, alomofu. Kwa mfano, -esh-, -ish-, -z-, -lish-, -lesh-, -vy-, na -fy- ni alomofu za mofimu ya usababishi.

Zoezi

(1) Tofautisha kwa mifano dhana za uambishaji nyambulishi na uambishaji ambatizi.

(2) Bainisha mofu zinazounda maneno yafuatayo:       (a) lililonikera       (b) tutafahamiana       (c) walikikimbilia       (d) sababu       (e) magazeti       (f) hawajajadiliana

(3) Kwa kutumia mifano ya vitenzi vya lugha ya Kiswahili, bainisha alomofu za kauli ya utendea, utendeshi na kauli ya utendeka.

Kuchanganua sentensi

Dhana ya tungo

Kabla ya kuanza kuchanganua sentensi, ni muhimu kuelewa dhana ya tungo na aina zake kwani uchanganuzi wa sentensi unazingatia mgawanyo na uhusiano wa tungo ndogo zilizomo ndani yake.

Tungo ni kipashio cha kimuundo kinachotokana na uwekaji pamoja wa vipashio vidogovidogo ili kujenga kipashio kikubwa zaidi. Uwekaji pamoja wa vipashio huongozwa na kanuni za kisarufi za lugha inayohusika.

Tungo huweza kuwa neno au kifungu cha maneno chenye kutoa taarifa fulani. Tazama mifano ifuatayo:

(i) Anayecheza

(ii) Wanafunzi waliosajiliwa

(iii) Kijana mzuri

(iv) Sara alisafiri jana

Mifano yote iliyotolewa ni tungo lakini viwango vya kukamilika kwa taarifa zake ni tofauti. Tofauti hiyo inajitokeza katika maana na mpangilio wa maneno uliojenga tungo hizo. Kwa mfano (i) - (ii) ni tungo ambazo zinatoa taarifa lakini taarifa

Aina za tungo

Aina za tungo ni pamoja na: neno, kirai, kishazi na sentensi.

(a) Tungo neno

Neno katika lugha ya Kiswahili linaweza kusimama peke yake kama tungo na likatoa taarifa fulani.

Neno hili linaweza kuwa shina kama vile cheza na soma au muunganiko wa shina na viambishi kama inavyojitokeza kwenye nomino mwanafunzi au kitenzi analima.

Neno ndilo kipashio cha msingi cha kisintaksia na ndilo pia huwa msingi wa uundaji wa tungo nyingine kubwa zaidi yake.

(b) Tungo kirai

Kirai ni aina ya tungo yenye neno moja au zaidi ambayo uhusiano wake umejikita katika neno kuu.

Neno kuu katika kirai hutokana na aina za maneno. Aina hizo za maneno zinaweza kusimama peke yake kama kirai au kuandamana na maneno mengine kwa kuzingatia uhusiano maalumu baina ya maneno hayo na neno kuu. Kwa hiyo, katika Kiswahili, jina la kirai hutokana na aina ya neno kuu lililopo katika kirai hicho, ambacho ni neno la kwanza katika kirai.

Kwa mfano, kama neno kuu ni nomino, kirai kitaitwa kirai nomino na kama neno kuu ni kielezi, basi kirai kitaitwa kirai kielezi.

Aina za virai

Virai vinaweza kugawanywa katika aina mbalimbali kwa kuzingatia neno kuu.

Aina za maneno zinazotupatia aina za virai ni nomino, vivumishi, vitenzi, na vielezi.

Viwakilishi huingia katika kundi la kirai nomino.

Hivyo, viwakilishi na maneno mengine kama vile viunganishi na vihisishi hayaundi kirai.

Viunganishi hutumika kuunganisha virai.

Aidha, vihisishi havifungamani wala kushikamana na maneno mengine katika tungo za Kiswahili.

Hivyo, aina hizi za maneno haziwezi kuunda virai.

Kwa hiyo, tuna aina tano za virai katika lugha ya Kiswahili:

kirai nomino,

kirai kivumishi,

kirai kitenzi,

kirai kihusishi na

kirai kielezi.

Kirai nomino (KN)

Hiki ni kirai ambacho neno lake kuu ni nomino au kiwakilishi.

Hii ina maana kwamba nomino au kiwakilishi hutawala upatanisho wa kisarufi wa neno au maneno yanayoandamana nalo katika tungo inayo husika.

Maneno yaliyoundiwa kwa hati mlalo katika data ifuatayo ni mifano ya virai nomino.

(i) Gari kubwa limerudishwa.
(ii) Gari kubwa kuliko yote limerudishwa.
(iii) Gari kubwa lililokuwa juu ya mlima limerudishwa.
(iv) Gari lililogongwa limerudishwa.

Miundo ya kirai nomino

Kirai nomino huwa na miundo mbalimbali kama inavyooneshwa katika sehemu zinazofuata.

Kwa kila muundo, mifano umeoneshwa kwa hati mlalo.

(a) Nomino moja peke yake

(i) Mwanamichezo amependeza.
(ii) Mtoto unacheza vizuri.
(iii) Shule imefunguliwa leo.

(b) Nomino mbili au zaidi zilizounganishwa na kiunganishi

(i) Baba, mama na kaka wamesafiri leo.
(ii) Juma na Roza wanapendeza sana.
(iii) Mjomba, shangazi na binamu watawasili kesho.

(c) Kiwakilishi kimoja au zaidi

(i) Wao walifika mapema sana.
(ii) Sisi tunasisitiza kwamba tutakuja.
(iii) Huyu na yule wanalima vizuri.

(e) Nomino na kivumishi kimoja au zaidi

(i) Mtu mzuri anacheza.
(ii) Mbwa mweupe mweupe amepotea.
(iii) Mzee ndogo fupi imefunikwa vizuri.
(iv) Magari mawili makubwa yanakuja.

(f) Nomino na kishazi rejeshi

(i) Wanafunzi waliokija jana wameitwa.
(ii) Kalamu iliyovunjika ni yangu.
(iii) Redio iliyonunuliwa imeibwa.
(iv) Karatasi zilizoletewa leo ni nzuri sana.

(g) Kitenzi-jina na kivumishi au bila kivumishi

(i) Kucheza kwako kutaleta balaa.
(ii) Kulima kule kunapendeza.
(iii) Kula kuzuri kumeshamiri kijijini kwetu.
(iv) Kusoma kunaburudisha.

Kirai kivumishi (KV)

Hiki ni kirai ambacho neno lake kuu ni kivumishi.

Kirai hiki kina miundo ifuatayo:

(a) Kivumishi peke yake. Kwa mfano:

(i) Wanafunzi wazuri wanahudhuria darasani.
(ii) Mtu mnene anakaribia baratibu.
(iii) Mwalimu hodari huwahimiza wanafunzi wasome.
(iv) Mbuzi mweusi amepelekwa mnadani.

(b) Kivumishi na kielezi

(i) Chakula ni kitamu mno.
(ii) Mboga ni nzuri sana.
(iii) Mtoto mweupe sana amekuja.
(iv) Mvulana mrefu zaidi ananike nguo.

(c) Kivumishi na kivumishi. Kwa mfano:

(i) Mtoto wetu mwerevu atafaulu masomo.
(ii) Watoto kumi warefu walifika shuleni.
(iii) Mbuzi mnoga mnene atachinjwa kesho.
(iv) Mtoto wangu mfupi anapenda kucheza mpira.

(d) Kivumishi na kishazi rejeshi. Kwa mfano:

(i) Kijana shupavu aliyeshinda tuzo amefika.
(ii) Msichana msafi ambaye amedhamiri kuwa balozi ni Nyembezi.

(e) Kivumishi na kirai kihusishi. Kwa mfano:

(i) Mzee maarufu kwa wizi amekamatwa.
(ii) Simba dume mwenye masharubu meusi amepotea.

Kirai kitenzi (KT)

Hii ni aina ya kirai ambacho neno lake kuu ni kitenzi. Hii ina maana kwamba muundo wake umeegemea katika uhusiano wa kitenzi na neno au mofimu mengine ya maneno katika tungo. Kirai hiki huundwa na neno la kitenzi kwa sababu hilo ndilo neno lake kuu.

Kirai kitenzi kina miundo ifuatayo:

(a) Kitenzi kimoja au zaidi

(i) Watoto wanasoma.
(ii) Watalii walikuwa wamepumzika.
(iii) Mwenyekiti atakuwa anakuja.
(iv) Mwalimu amefundisha.

(b) Kitenzi na nomino moja au zaidi (na kivumishi)

(i) Malima anapenda maua.
(ii) Dada alimpigia mgeni zawadi.
(iii) Anna alimuandalia mgonjwa msunda.
(iv) Waziri Mkuu alisoma hotuba.
(v) Dada anapika chakula kitamu.

(c) Kitenzi na kielezi

(i) Baba anatembea polepole.

(ii) Mbuzi anakula harakaharaka.

(iii) Mama amekwenda sokoni.

(d) Kitenzi na kivumishi

(i) Walimu ni wabunifu.

(ii) Jadia ni mpole.

(iii) Antonio hapendi wazembe.

(iv) Mti huu si mrefu.

Kirai kihusishi (KH)

Hiki ni kirai ambacho neno lake kuu ni kihusishi. Kihusishi hutokea katika sentensi kikiwa kimekamilishwa na nomino. Rejelea mifano ifuatayo:

(i) Mzee Honoye anakula kwa kijiko.

(ii) Mama amenunua gari la watoto.

(iii) Kijana ameleta majani ya ng'ombe.

(iv) Huu ni mwezi wa mvua.

(v) Kitabu chenye kurasa nyingi.

Kirai kielezi (KE)

Hiki ni kirai ambacho neno lake kuu ni kielezi. Kielezi huweza kukaa peke yake au kuambatana na kielezi kingine.

Aidha, kielezi katika tungo huweza kuelezea kitenzi, kivumishi au kielezi kingine. Tazama mifano ifuatayo:

(i) Ntekaniwa anatembea polepole sana.

(ii) Mwalimu atakuja kesho asubuhi.

(iii) Alijigonga mbele ya gari.

(iv) Dada amechoka sana.

(v) Kesho asubuhi, tukutane katika ukumbi huu.

Zoezi

1. Fafanua dhima ya neno kuu la kirai katika mawasiliano.

2. Kirai nomino kina dhima mbalimbali katika sentensi. Thibitisha kauli hii kwa hoja zisizopungua tano na mifano maridhawa ya Kiswahili.

3. Fafanua miundo mbalimbali ya kirai kitenzi kwa kutumia mifano ya Kiswahili.

4. Neno linaweza kuwa tungo ila si kila tungo ni neno. Jadili kauli hii kwa mifano ya Kiswahili.

Tungo kishazi

Kishazi ni tungo ya ngazi ya juu kuliko kirai na ya chini kuliko sentensi.

Kishazi kinaweza ama kuwa na maana kamili au maana isiyo kamili kutegemeana na kitenzi kilichomo katika kishazi hicho.

Kitenzi ni kipashio cha msingi katika kishazi. Kitenzi kinaweza kujitosheleza, yaani, kuwa na maana kamili, au kutojitosheleza na kutegemea kitenzi cha kishazi kingine ili kukamilisha maana.

Kwa msingi huo, tunaweza kupata aina mbili za vishazi. Aina hizo ni:

kishazi huru

kishazi tegemezi

Kishazi huru

Hiki ni kishazi kinachoweza kujitosheleza kimaana na kusimama peke yake kama sentensi. Hutambulishwa kwa alama KHr.

Ifuatayo ni mifano ya vishazi huru:

(i) Tukila vizuri tutakuwa na afya njema.

(ii) Ukiona mto umejaa maji, usivuke.

(iii) Chakula kilichopikwa jana, kilikuwa na ladha nzuri.

(iv) Dada anapika chakula anapokuwa nyumbani.

Miundo ya kishazi huru

Kishazi huru kina miundo mbalimbali kama ifuatavyo:

(a) Kitenzi kikuu pekee yake. Kwa mfano:

(i) Alicheza.

(ii) Tunalima.

(iii) Wanakimbizana.

(iv) Wataondoka.

(b) Nomino, kitenzi kikuu na nomino. Kwa mfano:

(i) Mama anapika ugali.

(ii) Mtoto ancheza mpira.

(iii) Diririja anatengeneza kinyago.

(iv) Manase anapiga gitaa.

(c) Nomino na kitenzi kikuu. Kwa mfano:

(i) Redio imeharibika.

(ii) Kiswahili kinakua.

(iii) Ng’ombe amezaa.

(d) Nomino, kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu.

Kwa mfano:

(i) Mama alikuwa anapika.

(ii) Mgonjwa atakuwa amelala.

(iii) Mwalimu alikuwa anafundisha.

(e) Nomino/kiwakilishi, kitenzi kishirikishi na nomino na /au kivumishi/. Kwa mfano:

(i) Joel ni mtoto mzuri.

(ii) Hii ni nchi kubwa.

(iii) Manka ni mama yangu.

(iv) Twiga ndiye mnyama mrefu.

Sifa za kishazi huru

Kishazi huru, kama kipashio cha msingi katika tungo, kina sifa mbalimbali ambazo huweza kutumika kukibainisha. Sifa hizo ni kama zifuatazo:

(a) Hujitosheleza kimuundo na kimaana.

(b) Kina sifa ya kuwa sentensi sahili.

(c) Hukamilisha taarifa ya kishazi tegemezi.

Kishazi tegemezi

Hiki ni kishazi ambacho hakiwezi kutoa maana kamili mpaka kikamilishwe na kishazi huru.

Kwa hiyo, kishazi tegemezi huacha maswali kwa msomaji kutokana na kutokamilika kwake. Hivyo, huhitaji kukamilishwa ili kuondoa maswali hayo.

Kishazi tegemezi hutambulishwa kwa alama KTg au β. Tazama mifano ifuatayo:

(a) Maswali yaliyosahihishwa ...

(b) Samaki waliovuliwa ...

(c) Alivyoingia ...

(d) Kwa sababu alikuwa mchangamfu ...

Miundo ya vishazi tegemezi vya Kiswahili

Lugha ya Kiswahili ina miundo minne ya vishazi tegemezi:

(a) Vishazi tegemezi vyenye muundo wa viunganishi tegemezi Vishazi tegemezi hivi hutokana na kuwapo kwa viunganishi tegemezi kama vile ingawa, ijapokuwa, isipokuwa, ikiwa, kwa kuwa, na kwa vile. Ifuatayo ni mifano ya vishazi tegemezi vya aina hiyo (vimeandikwa kwa hati mlalo):

(i) Kwa kuwa wanafunzi wanajisomea kwa bidii, watafaulu mitihani yao.

(ii) Hakuruka juu sana, ijapokuwa alikuwa mwepesi.

(iii) Ingawa alikuwa mrefu, hakuweza kuudaka mpira.

(iv) Ikiwa wananchi tutashirikiana kuwalinda tembo, vizazi vyetu vitanufaika kwa utalii.

(v) Mlifaulu vizuri, kwa vile mlikuwa mnasoma kwa bidii.

(b) Vishazi tegemezi vyenye muundo wa mofu za masharti Hizi ni mofu zinazodokeza hali ya masharti.

Mfano wa mofu hizo ni -ki-, -nge-, -ngeli- na -ngali-. Chunguza mifano ifuatayo (mofu za masharti zimeandikwa kwa hati mlalo):

(i) Akinipa pesa zangu, nitanunua vitabu.

(ii) Utaadhibiwa na mwalimu, ukishindwa kufuata taratibu za shule. (iii) Wangeondoka mapema, wangewahi kufika ukumbini.

(iv) Ungelikuwa na pesa ungelinunua gari.

(v) Angalikuwa mwaminifu angalipewa mtaji mkubwa.

(c) Vishazi tegemezi vyenye kwamba na kuwa Kwa mfano:

(i) Kusema kwamba hatupendi wali ni kusema uongo.

(ii) Kudai kuwa chakula hakitoshi kutasababisha matatizo.

(d) Vishazi tegemezi vyenye mofu za urejeshi

Aina hii ya muundo wa vishazi tegemezi hutokana na kupachika mofu za urejeshi katika vitenzi au baada ya neno amba-. Kwa mfano:

(i) Walimu wanaofundisha kwa juhudi watapewa zawadi.

(ii) Daraja lililobomoka limejengwa.

(iii) Kitabu ambacho kimeletwa ni kizuri.

(iv) Mwanafunzi aliyefaulu mitihani atajiunga na chuo kikuu.

(v) Michezo ambayo itafanyika mwaka huu itawavutia wengi.

Kitenzi cha kishazi tegemezi kinachotokana na mofu za urejeshi hushushwa hadhi na kufanya kazi ya kivumishi au kielezi.

Kwa hiyo, kutokana na mofu za urejeshi, tunapata aina anuwai za vishazi rejeshi.

(a) Vishazi virejeshi vinavyorejelea nomino/viwakilishi. Kwa mfano:

Watu walioumia wamepona.

Miti ambayo imekatwa ilikuwa barabarani.

Wanafunzi waliosimama mstari wa mbele wasogee mbele hatua moja.

Mkulima alimaye kwa bidii hupata mazao mengi.

(b) Vishazi rejeshi vinavyoonesha wakati. Kwa mfano:

Mwanahawa alifurahi sana alipofika mteja muda wa saa sita.

Baba alipokuja tulifurahi sana.

Wakati alipokuwa kijana nilimfahamu vyema.

(c) Vishazi rejeshi vinavyoonesha mahali. Kwa mfano:

Mahali panapopendeza ni hapa.

Mahali mlimoingia ni salama.

Kule kunakopendeza hakuna wadudu.

(d) Vishazi rejeshi vinavyoonesha namna/jinsi. Kwa mfano:

Watu walishangaa alivyoingia.

Kabula hakuolewa alivyoachiwa na basi.

Tulivyoondoka tuliwashangaza.

Sifa za vishazi tegemezi

(i) Havijitoshelezi kimaana. Hivyo, huhitaji vishazi huru ili kukamilisha maana.

(ii) Huundwa na:

(a) viambishi rejeshi;

(b) mofu za masharti;

(c) viunganishi tegemezi; na

(d) maneno kwamba au kuwa.

(iii) Huweza kuondolewa katika sentensi bila kupoteza maana ya msingi ya sentensi hiyo.

(iv) Huweza kutanguliwa au kufuatwa na kishazi huru.

(v) Kishazi tegemezi kinaweza kufanya kazi kama ifanywayo na kielezi au kivumishi.

Zoezi

1. Fafanua aina za vishazi kwa kutumia mifano mbalimbali.

2. Kwa kutumia mifano, bainisha miundo ya vishazi tegemezi.

3. Onesha vishazi tegemezi na vishazi huru kwa kutumia alama ( ) na [ ] katika sentensi zifuatazo:

(a) Hakutaka kabisa kumsikiliza Madebe kwa sababu ni muongo.

(b) Nitamwelewesha vizuri akinifuata.

(c) Kaka alichukua alipochomekwa.

(d) Miwani yangu ilipovunjika, nilishindwa kusoma.

(e) Aombaye hupewa.

Tungo Sentensi

Sentensi ni neno au kifungu cha maneno chenye kiima na kiarifu na hutoa taarifa iliyokamilika. Hiki ndicho kipashio kikubwa kabisa cha kimuundo katika tungo.

Sentensi huwa na muundo uliokamilika ambao hutoa taarifa kamili. Aidha, sifa ya kidhima au kiuamilifu inayotofautisha sentensi na vipashio vingine vya lugha ni kuwa na kiima (K) na kiarifu (A).

Sentensi huundwa na vipashio vingine vidogo ambavyo ni: 

neno

virai

vishazi.

Aina za sentensi

Uainishaji wa sentensi hufanywa kwa kutumia vigezo viwili:

- kigezo cha kimuundo

- kigezo cha kidhima

Kigezo cha kimuundo huzingatia mpangilio wa vipashio katika sentensi.

Kigezo cha kidhima huzingatia uamilifu wa vipashio vya sentensi.

Uainishaji wa sentensi kimuundo

Katika kigezo hiki, sentensi huainishwa kwa kuangalia vipashio vilivyounda sentensi na uhusiano uliopo baina ya kipashio kimoja na kingine.

Uhusiano wa vipashio katika sentensi hurejelea namna vipashio vya sentensi vinavyoshikamana, vinavyotegemeana na kutawalana katika kuunda sentensi.

Kuna aina tatu za sentensi kwa kuzingatia kigezo cha kimuundo 

sentensi sahili

sentensi ambatano

sentensi changamano

Sentensi sahili

Hizi ni sentensi ambazo huundwa na kishazi huru kimoja. Sentensi za aina hii huwa na wazo kuu moja. Kimsingi, usahili wa sentensi sahili hutokana na sentensi kuwa na taarifa moja, ambayo hubebwa na kitenzi kamili.

Ikiwa sentensi ina vitenzi zaidi ya kimoja vyenye taarifa tofauti, basi sentensi hiyo haitakuwa sahili.

Sentensi sahili ndiyo msingi wa uundaji wa sentensi nyingine.

Ifuatayo ni mifano ya sentensi sahili:

(i) Doto ana watoto wawili.
(ii) Mwalimu anaandika ubaoni.
(iii) Baba yangu alikuwa mkali.
(iv) Kaka alikuwa anaimba.
(v) Rais anahutubia wananchi wake.

Miundo ya sentensi sahili

Sentensi sahili huundwa na kitenzi kimoja au zaidi kinachodokeza wazo kuu moja.

Kwa kuzingatia ujitokezaji wa vitenzi katika tungo, sentensi sahili zinaweza kugawanywa katika miundo ya aina tatu ambayo ni: 

(a) Kitenzi kikuu peke yake

Katika lugha ya Kiswahili, kitenzi kikuu kinaweza kusimama peke yake na kuunda sentensi sahili.

Aidha, kitenzi kikuu kinaweza kuambatana na aina nyingine za maneno. Tazama mifano ya sentensi zifuatazo:

(i) Anaimba.
(ii) Anatembea polepole.
(iii) Tunasoma kitabu.
(iv) Anaogelea kwenye bwawa.

(b) Kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu

Muundo huu unaonyesha kitenzi kisaidizi kimoja au zaidi na kitenzi kikuu. Vilevile, vitenzi hivyo vinaweza kuandamana na maneno mengine katika sentensi. Tazama mifano hapa chini:

(i) Dereva atakuwa amepanga miti.
        

(ii) Dada alikuwa anapenda nyimbo.
     

(iii) Baba alikuwa analima.     

(c) Kitenzi kishirikishi

Muundo huu huwa na kitenzi kishirikishi ambacho huandamana na maneno mengine kuunda sentensi. Alama inayotumika kurejelea kitenzi kishirikishi ni t. Tazama mifano ifuatayo kwa kuzingatia vitenzi vishirikishi:

(i) Mtoto angali mgonjwa.
(ii) Juma na Paulo ni watoto wetu.
(iii) Maua yalikuwa machanga.
(iv) Maji safi yamo mtungini.
(v) Wao si wanafunzi.

Sentensi changamani

Hizi ni sentensi ambazo huundwa na kishazi tegemezi kimoja au zaidi na kishazi huru au vishazi tegemezi viwili vinavyokamilishana.

Vishazi hivi viwili au zaidi havivunganishwi kwa kutumia viunganishi. Tazama mifano ifuatayo:

(i) Mchezaji aliyecheza vizuri amepata zawadi.

(ii) Mgeni rasmi alipofika, sherehe ilianza rasmi.

(iii) Akifika tu, nitaarifu.

(iv) Kwa sababu alikuwa na adabu, watu wengi walimpenda.

(v) Angekua mwaminifu, angekabidhiwa duka la baba yake.

Miundo ya sentensi changamani

Sentensi changamani zina miundo miwili kama ifuatavyo:

(a) Kishazi tegemezi kimoja au zaidi na kishazi huru. Kwa mfano:

(i) Kiti kilichoharibika, tumemtengenezea.

(ii) Kila nilipokuwa nikitaka kumpiga, roho ilikataa.

(iii) Msichana aliyekuja juzi, akiwa amesuka nywele, amendoka na begi langu.

(iv) Babu aliyewasili leo, tulipokuwa tunakula ugali, anaitwa Mzee Kidimo.

(b) Vishazi tegemezi viwili vinavyokamilishana. Kwa mfano:

(i) Angesoma kwa bidii, angefaulu vizuri.

(ii) Angalianza matitabu mapema, angalipona.

(iii) Angelikuwa na sauti nzuri, angeliunga na kwaya ya shule.

Sentensi ambatani

Hizi ni sentensi ambazo huundwa na sentensi mbili au zaidi ambazo huunganishwa kwa kutumia kiunganishi. Kwa hiyo, aina hii ya sentensi ina taarifa zaidi ya moja. Kwa mfano:

(i) Mwalimu anafundisha na mwanafunzi anasikiliza.

(ii) Mtoto analia, mama anambembeleza na baba anamsaidia.

(iii) Dada anakuja leo na kaka atakuja kesho, lakini mjomba hatakuja kabisa.

(iv) Mwanafunzi aliyemaliza amepelekwa hospitalini na kijana aliyempiga ameadhibiwa.

(v) Kwa sababu hakuwa mwadilifu alifukuzwa shule mara moja, lakini wenzake waliendelea na masomo kama kawaida.

Miundo ya sentensi ambatani

Sentensi ambatani ina miundo mitatu kama inavyoonyeshwa hapa chini.

(a) Sentensi sahili mbili au zaidi. Kwa mfano:

(i) Mtoto anacheza na mama anafua nguo.

(ii) Dada ameenda kuchota maji na kaka ameenda mjini.

(iii) Mwalimu anafundisha lakini wanafunzi hawazingatii.

(iv) Gawile anafanya kazi ila Elimboto anategemea.

(v) Tulicheza vizuri lakini hatukufunga magoli wala hatukufungwa.

(b) Sentensi changamani na sentensi sahili. Kwa mfano:

(i) Watoto waliosafiri wamerudi, ila wamesahau mizigo yao.

(ii) Mtoto aliyefanya vizuri amekuja, lakini hajafika na mitihani yake.

(iii) Ingawa leo ni siku ya mnada, hakuchinja ng’ombe, bali amechinja mbuzi.

(iv) Akifika nitampa chakula isipokuwa sitampa kinywaji.

(c) Sentensi changamani mbili au zaidi. Kwa mfano:

(i) Kijana aliyevaa shati jekundu ni mwanafunzi, lakini yule aliyevaa shati jeupe ni kaka yangu.

(ii) Akija kwangu nitamsikiliza, lakini asipokuja sitamtafuta.

(iii) Kwa sababu alikuwa anaimba harakaharaka, sikupenda uimbaji wake, ila kucheza kwake kulinivutia.

(iv) Iwapo atakuuliza maswali, mwelekeze kwangu, lakini asipokuuliza usimwelekeze.

Uainishaji wa sentensi kidhima

Kigezo hiki cha uainishaji wa sentensi hujikita katika uamilifu ambao umebebwa na sentensi inayohusika.

Katika uainishaji huu, tunaangalia kama sentensi inatoa taarifa, amri, inauliza swali, au inadokeza hali ya mshangao.

Kwa hiyo, sentensi zinazoainishwa kwa kutumia kigezo cha kidhima ni: 

sentensi amrishi/agizi,

sentensi arifu,

sentensi ombi,

sentensi ulizi,

na sentensi mshangao

1. Sentensi amrishi/agizi

Hizi ni sentensi ambazo hutoa maelekezo ya kutendeka kwa jambo fulani.

Katika aina hii ya sentensi, msemaji ndiye mwamuzi, na mtendaji hutajwa/atajwe kuelekeza agizo.

Katika sentensi amrishi, kitenzi huwa na umbo la shina na katika wingi hubeba kiambishi -ni katika uyakinishi.

Katika ukanushi, hubeba kiambishi cha nafsi na kiambishi cha wakati/nyakati cha ukanushi.

Hizi ni sentensi za kutoa amri.

(i) Nendeni!

(ii) Ondoka!

(iii) Nenda darasani!

2. Sentensi ombi

Hizi ni sentensi ambazo humtaka mtu mwingine akubali kutenda jambo fulani.

Sentensi za ombi hutumia sifa ya upole. Katika sentensi za ombi, kitenzi huanza kwa nafsi ya pili umoja au wingi, na irabu tamati hubadilika na kuwa -e katika vitenzi vyenye asili ya Kibantu. Tazama mifano ifuatayo:

(i) Unisadie chenji.

(ii) Tafadhali mniombee.

(iii) Unifikirie vizuri.

3. Sentensi arifu

Hizi ni sentensi ambazo hutoa taarifa kuhusu jambo fulani. Tazama mifano ifuatayo:

(i) Mheshimiwa Rais atawasili kesho asubuhi.

(ii) Baba yao ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya.

4. Sentensi ulizi

Hizi ni sentesi ambazo huuliza. Hivyo, ni sentensi ambazo huwa na pengo linalohitaji jibu la taarifa fulani.

Sentensi hizi huisha kwa alama ya kuuliza. Kwa mfano:

(i) Mama atarudi lini?

(ii) Mmeelewa?

5. Sentensi mshangao

Hizi ni sentensi ambazo huonesha kustajabu, au kushikwa na butwaa.

Sentensi hizi huishia kwa alama ya mshangao.

Kwa mfano:

(i) Hee! Hata yeye amechaguliwa!

(ii) Kumbe! Halipi kodi!

Zoezi

1. Andika mazungumzo ya watu wawili kuhusu mada yoyote na upigie mstari sentensi changamani kumi katika habari hiyo.

2. Kwa kutumia mifano ya Kiswahili, fafanua namna sentensi ambatani zinavyoweza kujitokeza?

3. Tumia maneno ingawa, ijapokuwa, hata hivyo, na isipokuwa kutunga sentensi ambatani.

Uchanganuzi wa sentensi

Uchanganuzi wa sentensi ni uchambuzi wa sentensi kwa kubainisha vipashio vyake vya kimatumizi au kidhima.

Katika kubainisha vipashio vya sentensi, tunaweza kuvipanga vikawa katika vikundi.

Uchanganuzi wa sentensi za Kiswahili huongozwa na mikabala miwili:

Mkabala wa kidhima

Mkabala wa kimuundo

Uchanganuzi wa sentensi unafanana kwa mikabala yote, isipokuwa istilahi zinatofautiana.

Uchanganuzi wa sentensi zinazohusiana na mikabala yote miwili inaweza kutumiwa kwa kuchanganya.

Mkabala wa kidhima

Mkabala huu huchanganua uamilifu wa vipashio vinavyounda sentensi. Kwa hiyo, unatumia istilahi za kidhima zifuatazo:

(a) Kiima

Kiima ni kipashio cha kiuamilifu cha sentensi ambacho hufafanuliwa na kitenzi.

Sehemu ya kiima huweza kukaliwa na nomino, kiwakilishi, au kifungu kingine cha maneno kinachofanya kazi kama nomino.

Katika sentensi za kauli ya kutenda, kiima huwa mtenda wa jambo.

Kiima hutambulishwa kwa alama K.

Chunguza mifano ya kiima katika mifano ifuatayo:

(i) Mtoto mdogo analia.
(ii) Mbwa amecharazwa viboko.
(iii) Nguo zimefuliwa vizuri.

Vipashio vya kiima

(a) Nomino moja au zaidi au nomino na kivumishi. Kwa mfano:

(i) Paka amekamata panya.
(ii) Mariamu na Hamida walifika kwenye sherehe.
(iii) Kaka mkubwa anacheza mpira.
(iv) Mtoto mzuri umefaulu mtihani.
(v) Mwalimu Mweledi anafundisha.

(b) Kiwakilishi peke yake au kiwakilishi na kivumishi. Kwa mfano:

(i) Yule analima sana.
(ii) Wao watakuja kesho.
(iii) Yule mrefu ni kaka yetu.
(iv) Wale wanne walikuja jana.

(c) Nomino na kishazi rejeshi. Kwa mfano:

(i) Mtoto aliyekuja leo amefaulu.
(ii) Kiatu kilichopotea kimeonekana.
(iii) Msichana aliyevaa vizuri ni rafiki yangu.
(iv) Kicheko ambacho alicheka kilinishtua.

(d) Kitenzi-jina na kivumishi. Kwa mfano:

(i) Kucheka kwao kuliwafurahisha wote.
(ii) Kupotea kwake kuliwaumiza wengi.
(iii) Kukimbia kule hakukuwa kwa kawaida.

(b) Kiarifu

Hiki ni kipashio cha kiuamilifu katika sentensi ambacho kina kitenzi ndani yake na kinafafanua kiima.

Kipashio kikuu cha kiarifu ni kitenzi.

Kiarifu hutokea upande wa kulia.

Kiarifu hutambulishwa kwa alama ya herufi A.

Vipashio vya kiarifu

(a) Kitenzi (T)

(i) Mtoto anacheza vizuri.
(ii) Juma ni mrefu.
(iii) Anacheza.
(iv) Yeye hucheza kila jioni.
(v) Mwanafunzi alikuwa anaumwa.

(b) Shamirisho (SH) au kijalizo

Shamirisho ni sehemu ya kiarifu ambayo hukaliwa na mtendwa au mtendewa.

Mtendwa hujulikana pia kama yambwa na mtendewa hujulikana pia kama yambiwa.

Yambwa ni kipashio ambacho huathiriwa na tendo.

Yambiwa ni muafaka wa tendo linaloelekezwa na kitenzi.

Dhima ya shamirisho ni kukamilisha taarifa inayolekezwa na kitenzi.

Vitenzi elekezi ni vitenzi vinavyobeba yambwa au yambiwa. Kwa mfano:

(i) Jana tulichinja mbuzi wawili.
(ii) Kaka amemjengea baba nyumbа kubwa.
(iii) Mwalimu amewaonyesha wanafunzi vitabu vipya.
(iv) Raina amempa Ndola ukwaju mtamu sana.
(v) Baba amemnunulia dada nguo nzuri.

Katika lugha ya Kiswahili, kitenzi kikiitwa kinahitaji kukamilishwa kwa nomino mbili basi nomino ya kwanza ni yambiwa na nomino ya pili ndiyo yambwa.

(c) Chagizo (CH)

Chagizo ni sehemu ya kiarifu ambayo hukaliwa na kielezi. Kielezi kinaweza kuhamahama katika sentensi bila kuathiri maana. Kwa mfano:

(i) Mwalimu aliwaambia wanafunzi waondoke upesi.

(ii) Ngoswe alikimbia mapema.

(iii) Unapenda kula polepole.

(iv) Abel anachora ubao.

Aidha, vielezi vinaweza kuhamahama katika sentensi. Kwa mfano:

(i) Leo nitakula ugali.

(ii) Nitakula ugali leo.

Uchanganuzi wa sentensi kidhima hufuata hatua mbalimbali ambazo huanzia katika kipashio kikubwa kabisa kwenda kipashio kidogo.

Hatua za uchanganuzi wa sentensi kidhima

(i) Kubainisha aina ya sentensi ili kujua vipashio vinavyounda sentensi hiyo. Aina za sentensi katika mkabala wa kidhima ni sentensi arifu, amrishi, ulizi na mshangao.

(ii) Kubainisha vipashio vinavyounda sehemu kuu mbili za sentensi. Katika mkabala wa kidhima, vipashio hivyo ni kiima (K) na kiarifu (A).

(iii) Kubainisha vipashio vinavyounda kiima na kiarifu ambavyo kwa upande wa mkabala wa kidhima, ni nomino (N) au kiwakilishi (W) na kivumishi (V) katika kiima, na kitenzi (T), shamirisho (SH) na chagizo (CH) katika kiarifu.

(iv) Kuandika aina za maneno zilizomo katika sentensi inayohusika. Aina hizo huandikwa kwa kutumia vifupisho vya aina za maneno kama vile N, T, V, E, W, H, na U. Hii hutumika kwa namna sawa katika mikabala yote ya uchanganuzi.

Chunguza mifano ifuatayo:

Njia ya maelezo

(i) Sentensi ulizi

Maziwa ni lishe bora?

Hii ni sentensi ulizi.

Sentensi hii imeundwa na kiima na kiarifu.

Kiima kimeundwa na nomino.

Nomino ni maziwa.

Kiarifu kimeundwa na kitenzi kishirikishi na shamirisho.

Kitenzi kishirikishi ni ni.

Shamirisho imeundwa na nomino na kivumishi.

Nomino ni lishe.

Kivumishi ni bora.

(ii) Sentensi arifu

Wanafunzi wanafagia darasani na wengine wanapanga viti.

Hii ni sentensi arifu.

Sentensi arifu imeundwa na sentensi mbili zilizounganishwa na kiunganishi na.

Sentensi ya kwanza imeundwa na kiima na kiarifu.

Kiima kimeundwa na nomino.

Nomino ni wanafunzi.

Kiarifu kimeundwa na kitenzi na chagizo.

Kitenzi ni wanafagia.

Chagizo imeundwa na kielezi.

Kielezi ni darasani.

Kuna kiunganishi na.

Sentensi ya pili imeundwa na kiima na kiarifu.

Kiima kimeundwa na kiwakilishi.

Kiwakilishi ni wengine.

Kiarifu kimeundwa na kitenzi na shamirisho.

Kitenzi ni wanapanga.

Shamirisho imeundwa na yambwa.

Yambwa ina nomino.

Nomino ni viti.

Njia ya matawi

(Mifano ya Uchanganuzi inapatikana katika 'pdf' wasiliana na Mwalimu Kujipatia nakala yako WhatsApp 0653250566)

2. Mkabala wa kimuundo

Mkabala huu hutumika kuchanganulia sentensi kwa kuzingatia miundo ya vipashio vya sentensi.

Kwa hivyo, istilahi za kimuundo kama vile kirai nomino (KN), kirai kitenzi (KT), kirai kivumishi (KV), kirai kielezi (KE), na kirai kihusishi (KH) ndizo hutumika katika uchanganuzi wa sentensi.

Uchanganuzi wa sentensi kimuundo

Uchanganuzi wa sentensi kimuundo hufuata hatua mbalimbali ambazo huanzia katika kipashio kikubwa kabisa kwenda kipashio kidogo. Hatua hizo ni hizi zifuatazo:

(i) Kubainisha aina ya sentensi ili kujua vipashio vinavyounda sentensi hiyo.

Katika mkabala wa kimuundo, kuna sentensi sahili, ambatani na changamani.

(ii) Kubainisha vipashio vinavyounda sehemu kuu mbili za sentensi, ambavyo ni kirai nomino (KN) na kirai kitenzi (KT).

(iii) Kubainisha vipashio vinavyounda kirai nomino (KN) na kirai kitenzi (KT). Vipashio vinavyounda kirai nomino (KN) ni nomino (N) au kiwakilishi (W) kifuatiwa na kirai kivumishi (KV) au kishazi rejeshi (KR). Vipashio vinavyounda kirai kitenzi (KT) ni kitenzi (T) ambacho kinaweza kuambatana na kirai nomino (KN), kirai kivumishi (KV), kirai kielezi (KE), au vyote kwa pamoja.

(iv) Kubainisha vipashio vyote vinavyounda virai katika sentensi inayohusika ambavyo ni aina za maneno zinazowakilishwa kwa vifupisho N, T, V, E, W, H, U, na kadhalika.

Mkabala huu huzingatia njia zote za uchanganuzi wa sentensi kama ifuatavyo:

 (Mifano ya Uchanganuzi inapatikana katika 'pdf' wasiliana na Mwalimu Kujipatia nakala yako WhatsApp 0653250566)

Zoezi

1. Eleza changamoto unazokutana nazo wakati wa uchanganuzi wa sentensi kwa kila njia ya uchanganuzi uliyojifunza.

2. Fafanua kwa mifano mitatu hatua za uchanganuzi wa sentensi kimuundo.

Changanua sentensi zifuatazo kwa njia ya matawi na ya jedwali kwa kutumia mkabala wa kimuundo:
(a) Kasabanya amempa Ruboza karatasi.
(b) Msichana aliyekuja jana ameondoka leo.
(c) Mama anapika na baba anaosha vyombo.
(d) Sisi tulikubali makosa ila wao walikataa.

Tamrini

1. Uchambuzi wa miundo ya sentensi una umuhimu gani kwa mtumiaji wa lugha?

2. Sentensi changamani zina miundo mbalimbali. Bainisha miundo hiyo kwa mifano ya Kiswahili.

3. Kitenzi cha Kiswahili kina ukwasi wa viambishi vya kisarufi. Fafanua ukweli huu kwa kutumia mifano maridhawa.

Popular posts from this blog

SMS 20 za Mahaba Makali Kumtumia Mpenzi Wako

SMS 20 za Vichekesho Zinazochekesha Sana

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie