Posts

Showing posts with the label riwaya

Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tano

Image
  Aliweza kuwatambua watu hao. Mmoja aliitwa Sasi, kosa lake Wizi. Wala hakusingiziwa. Sasi alikuwa mwizi aliyechukiwa na watu wote. Wa pili alikuwa Athu, yeye alifungwa kwa kosa la uharifu kama Sasi. Naye hakusingiziwa, alikuwa mwizi wa mifugo aliyechukiwa na wafugaji wote. Wa tatu aliitwa Sipe, alifungwa kwa hofu ya mfalme. Mfalme alimuogopa Sipe kuwa ipo siku angempindua. Sipe alikuwa mtu mwenye maneno ya busara. Mara chache alitabiri mambo yakatokea, hii ilimpa hofu mfalme kwa kuona Sipe atapendwa na watu kuliko yeye na kuleta mapinduzi. Sipe alionewa! “Hamjambo ndugu zangu?” Alisalimia Mako. “Hatujambo,” walijibu. Sipe akaendelea, “Hakuna aliyesalama, hata wewe Mako umeletwa humu? Umefanya kosa gani hasa?” “Ni uonevu tu,” alijibu Mako, akikaa katika kitanda cha majani, “nina mvua mbili za kunifanya niendelee kuwa hai. Nimehukumiwa kunyongwa kwa kosa la kuonekana katika ndoto ya malkia. Malkia kaota kwa sauti akisema ananipenda na hawezi kuniacha milele!” Wote walicheka, l

Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Nne

Image
  Haikupita muda, Mako aliletwa kwa mfalme akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wapandao punda. Alishushwa, naye kwa heshima akapiga mguu wa kuume mara tatu kumsalimu mfalme. Mfalme hakujibu salamu hiyo. alimtazama kwa ghadhabu Mako. Baraza lilikaa ili kusikiliza mashtaka. Mako alivalia shati kubwa la buluu , suruali pana kiasi na viatu imara vya ngozi. Jamii ya Kanakantale, haikuwa nyuma katika teknolojia ya mavazi, watu wake walivaa mavazi ya kisasa! Mfalme alianza kusoma mashtaka, “Mako, mkulima, mfugaji na muwindaji, unatuhumiwa kwa kosa la kujihusisha na mahusiano na mke wa mfalme, yaani Malkia wa nchi ya Kanakantale. Usiku tukiwa tumelala, nilisikia kwa masikio yangu Malkia akitamka kuwa anakupenda na anaahidi kuwa wako daima. Japo Malkia alikuwa ndotoni, haimaanishi kuwa huna mahusiano naye. Kinachotokea ndotoni ni matokeo ya kilichotendeka mchana. Una chochote cha kujitetea?” “Mfalme wangu,” alijibu Mako, “nimekosa nini hata niwe na mahusiano na Malkia wa nchi yangu? Nar

Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Tatu

Image
  “Ndugu zangu,” alisema kwa sauti kubwa, “Wanaume msijifungie ndani, njooni nje twende tukapambane na huyu Simba. Mkiendelea kubaki ndani hakuna atakayesalia kwa sababu milango yetu siyo imara kiasi cha kumzuia asiivunje. Ni heri tufe tukipigana naye kuliko tujifungie ndani naye aje atukamate kama mwewe akamatavyo vifaranga. Je mnavyakula vya kutosha siku ngapi? Sasa hamuoni mnawindwa na njaa pamoja na simba? Aliyetayari kupambana ajitokeze sasa.” Zilipita dakika tisa tangu azungumze maneno hayo. Hakuna mwanamume aliyetoka ndani kuja nje kuungana naye, Bwana Mako akaamua kuingia msituni peke yake kumsaka Simba mzee. Akiwa anatembea alirushiwa mkuki. “Chukua mkuki huo utakusaidia kupambana na simba huyo,” ilisema sauti kutoka nyumba moja, kisha ikasikika sauti ya kufunga mlango, pakawa kimya. “Ni uonevu kumuua simba mzee kwa mkuki, simba mzee anauliwa kwa viganja vitupu!” alijibu Bwana Mako kisha akapotelea msituni. Wanakijiji walichungulia katika madirisha yao kama wanaoangal

Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Pili

Image
“ Katika kijiji kimoja cha kijani, waliishi watu wenye furaha. Furaha yao ilidumu kwa miaka mingi mpaka walipovamiwa na simba mmoja mzee. Simba huyu mzee, alikuwa katili kwa wanakijiji, kijiji kikakosa amani na furaha yao ikateketea kama fedha za mlevi ziteketeavyo baa. Simba mzee alianza unyama wake kwa kumuua mzee maarufu wa kijiji aliyependwa na watu wote. Inasemekana kuwa mzee alikuwa katika shamba lake akipalilia mahindi, ndipo alipovamiwa na simba mzee ambaye alimrukia shingoni na kumuua kisha akamla mpaka aliposhiba na kuacha sehemu ndogo ya mwili. Simba mzee hakuishia hapo, aliwatafuna watoto wawili mapacha waliokuwa wakichoma viazi pembezoni mwa nyumba yao. Basi baada ya tukio hilo, habari ya simba huyo ikaenea kwa wanakijiji na kila mmoja akajifungia katika nyumba yake akiogopa kutoka kwa hofu ya yule simba mzee. Kwa kuwa wanakijiji walijifungia ndani, simba yule mzee alipohisi njaa, akawinda watu asiwaone, akaanzisha kioja kipya, alianza kubomoa nyumba za watu na kuwa

Mfalme Anataka Kuniua | Sehemu ya Kwanza

Image
  Mako alijibanza katika kichaka cha kijani. Mbele alitazama kundi kubwa la swala. Akapiga hesabu haraka yupi amkamate. Aliona swala watatu waliokuwa na watoto, hao hakutaka kuwakamata, asingependa kuwatenga swala wale wadogo na mama zao. Basi alitazama kwa makini akagundua uwepo wa swala mzee kuliko wengine, huyo akamuwekea lengo la kumkamata. Alichomoka katika chaka alilojificha kwa kasi kama Simba. Swala walikimbia, naye akamkimbiza mmoja aliyekuwa mzee, alitamani kwenda kumgeuza kitoweo, wadogo aliwaacha wafurahie dunia. Swala mzee alikimbia kama gari jipya, nayo mbuga ikatulia ikimtazama Mako na swala. Kona ya kwanza ilikatwa, Mako naye akakata, kona ya pili, chenga, kona ya tatu, hola, kona ya nne, imo! Swala akakamatwa. Mako aliwinda bila silaha, yeye alikimbiza wanyama kama wafanyavyo wanyama wengine wala nyama. Wakati yote hayo yakitokea, Malkia wa nchi ya Kanakantale alikuwa akishuhudia. Siku hiyo, yeye na wasaidizi wake, alikwenda porini kujionea wanyama. Alishangazwa

Niliugua Ugonjwa wa Ajabu Nikatibiwa na Babu wa Kichina 1

Image
Simulizi hii haina uhusiano wowote na tukio la kweli lililowahi kutokea, bali ni matokeo ya fikra adimu za Mwalimu Makoba. Tajiri Maige aliniita nyumbani kwake. Hii ilikuwa ni mara ya nane, kwa mara zote saba, ameniita asifanikiwe kunishawishi kwa jambo alilohitaji. Alihitaji kunituma nchi za mbali, niende uchina kwa kazi ya kumtafuta binti yake ambaye tangu aondoke nchini kwenda China kusoma, hajapata kurejea tena na sasa yapata mwaka wa saba. Hakuna barua, hakuna simu, hakuna mawasiliano! “Mako… Mako… Mako…” aliniita tajiri Maige, “safari hii sitegemei jibu la hapana. Kila kitu kipo tayari. Naomba sana, nenda kamtafute mwanangu wa pekee Vida.” Ukimya ulitawala kwa dakika saba sebuleni pale. Sikuwa tayari kwenda mbali na familia yangu, nilihitaji kupumzika na nilizichoka purukushani. Hata hivyo, nilijiwa na moyo   wa huruma, nikajikuta nikitamka kwa kauli thabiti. “Nitakwenda peke yangu. Nitarudi na binti.” Hivyo ndivyo nilivyokubali kuondoka nchini ili kwenda C

Bwana Mako na Ndege Yake 2 | Mikasa Elfu Moja ya Bwana Mako 4

Image
Mkasa wa Nne Bwana Mako na Ndege Yake Sehemu ya Pili Jitu lilifika nyumbani kwake likiwa limemuweka Bwana Mako mfukoni. Mke wa Jitu pamoja na watoto wake wawili, walikaa sebuleni. Jitu lilipoingia tu, watoto walilikimbilia wakifurahi kurejea kwa baba yao. Hata hivyo, Jitu halikuwa na furaha kwa sababu siku hiyo halikurudi na chochote cha kulisha familia. Kumbe Jitu lilikuwa masikini! Jitu lilisogea mpaka alipokaa mkewe, likamshika mkono wa utosi kuashiria kwamba halikufanikiwa kupata chochote. Mke wa Jitu asiye na maneno mengi, aliwaamuru watoto waingie vyumbani kulala kuisubiri kesho. Bwana Mako aliyaona yote haya akichungulia kutoka mfukoni mwa shati alimokuwa. Nalo jitu lilikwenda mpaka katika kitanda kikubwa likakaa na kumtoa. Bwana Mako asiye na hofu tena, aliliamuru Jitu limuweke sikioni apate kuliambia jambo. “Rafiki mwema,” Bwana Mako alianza kusema, “nimeona wewe ni masikini, kiasi kwamba huna chochote cha kulisha wanao. Lakini rafiki, nakuahidi kukufanya ta

Bwana Mako na Ndege Yake 1 | Mikasa Elfu Moja ya Bwana Mako 3

Image
Mkasa wa Tatu Bwana Mako na Ndege Yake Sehemu ya Kwanza Kwa muda mrefu Bwana Mako alitamani kuitembelea Dunia aione yote akiwa juu. Ndipo alipopata wazo la kutengeneza ndege ambayo ingemsaidia kutimiza malengo yake. Umbo la ndege lilitengenezwa kwa mbao za mninga, ndani aliweka furushi kubwa la nyasi ambalo lingetumika kama kiti cha rubani, nyuma ya kiti cha rubani aliweka godoro nene, hili lingetumika kulala pale anapokuwa amechoka na muda huo ndege ingekuwa katika ‘autopilot.’ injini za ndege hii na namna ilivyofanya kazi, ilikuwa siri yake Bwana Mako. Aliamka asubuhi kabla mkewe na mtoto wake mdogo hawajaamka. Aliandika ujumbe katika kikaratasi, “Nakwenda ziara, nitarudi baada ya siku tatu.” kisha akaelekea mpaka mahali alipoegesha ndege, akaingia humo, alipokaa vyema, akavuta kigingi cha kwanza, ndege ikaunguruma kwa sauti kubwa na kuanza kuserereka taratibu kama maharusi. Baadaye iliongeza kasi, ikaserereka kwa sekunde chache, kisha akavuta kigingi cha pili, ndege i

Watekaji | Mikasa Elfu Moja ya Bwana Mako 2

Image
Mkasa wa Pili Watekaji “Zaidi ya watoto elfu moja wametekwa na majambazi ambao wamedai hawawezi kuwaachia mpaka wapewe kiasi cha Shilingi Trilioni saba…” ilisikika taarifa ya habari katika redio ndogo aliyokuwa akisikiliza Bwana Mako mchana saa sita. Mako huishi mjini na kijijini, nchi kavu na majini, na mara chache angani. Leo alikuwa mjini alipopokea taarifa hiyo. “Juhudi za kuwaokoa zimegonga mwamba,” iliendelea taarifa, “watekaji wametishia kuwaua watoto wote endapo hawatalipwa fedha wanazotaka ndani ya dakika 30. Pia wametaja mfumo wa malipo hayo ufanyike kwa njia ya mtandao na malipo yawe katika Bitcoin.” Bwana Mako alitambua kuwa siku hiyo kulikuwa na sherehe iliyohusisha watoto wa viongozi na wafanyabiashara wakubwa nchini kwake. Watoto hao wa wakubwa, walikutana pamoja katika sherehe iliyohusisha michezo mingi ikiwemo kuogelea. Bwana Mako hakupenda sherehe za aina hizi kwa sababu kwake yeye hazikuwa na maana yoyote zaidi ya ubaguzi tu, kwani watoto wa hohehahe hawak

Bwana Mako na Simba Mzee | Mikasa Elfu Moja ya Bwana Mako 1

Image
Mikasa Elfu Moja ya Bwana Mako ni mkusanyiko wa hadithi tamu kuliko hadithi zote ulizowahi kusoma. Mwalimu Makoba kaandika hadithi hizi kwa miaka 10 mfululizo ili kuwafanya watu wapende kusoma. Anayesoma hupata faida hizi: kuchangamsha akili, kupunguza mawazo, kuongeza maarifa, kuwa na kumbukumbu na kuwa na kinga dhidi ya magonjwa ya akili! Mkasa wa Kwanza Bwana Mako na Simba Mzee Katika kijiji kimoja cha kijani, waliishi watu wenye furaha. Furaha yao ilidumu kwa miaka mingi mpaka walipovamiwa na simba mmoja mzee. Simba huyu mzee, alikuwa katili kwa wanakijiji, kijiji kikakosa amani na furaha yao ikateketea kama fedha za mlevi ziteketeavyo baa. Simba mzee alianza unyama wake kwa kumuua mzee maarufu wa kijiji aliyependwa na watu wote. Inasemekana kuwa mzee alikuwa katika shamba lake akipalilia mahindi, ndipo alipovamiwa na simba mzee ambaye alimrukia shingoni na kumuua kisha akamla mpaka aliposhiba na kuacha sehemu ndogo ya mwili. Simba mzee hakuishia hapo, aliwatafuna w