Dhima Tano za Mofimu KI Katika Lugha ya Kiswahili

Mti Mkubwa

Siku zote ambazo nilisimamia mitihani ya taifa, nilisimamia wanafunzi waliokuwa shule. Sikuwahi kusimamia wanafunzi wa kujitegemea mpaka ilipowadia mwaka fulani ambapo nilipangwa kwenda kusimamia mtihani wa taifa katika shule fulani ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Muda ulipowadia, nilifika katika kituo changu, baada ya kufuata taratibu zote, nilisimama pembezoni ya mti ili niweze kuwaona wanafunzi waliokuwa wakifika shuleni hapo tayari kufanya mtihani.

Alipita binti mmoja mrembo sana ambaye naye alikuwa miongoni mwa wale wanaofanya mtihani, kwa sababu ya urembo wake, nilikosa nguvu za kusimama na isingekuwa kuushikilia ule mti, ningedondoka! Hata hivyo, nilikaa katika hali ya kuhisi kizunguzungu kwa muda wa dakika tano, hali ilipokuwa shwari, nikaelekea darasani ambako ndipo mtihani ulikuwa ukifanyika.

Niliingia darasani, mimi na mwenzangu mmoja tuliyekuwa tunasimamia pamoja, tulitimiza taratibu zote na mtihani ulianza. Katika chumba hiki cha mtihani, yule binti mrembo sana, alikuwamo na alikaa siti za katikati.

Wakati mtihani ukiendelea, nilitembea hapa na pale, nikipiga jicho huku na kule ili kuhakikisha mtihani unafanyika kwa kufuata sheria hizi na zile.

Katika hali isiyo ya kawaida, yule binti mrembo sana, mara baada ya kukaribia alipokaa, alificha kitu kwa haraka, nami nilisogea kwa kasi ileile aliyotumia kuficha kile kitu, nikafunua karatasi yake na kuona karatasi moja ndefu isiyokuwa sehemu ya mtihani ambayo iliandikwa baadhi ya mada za somo la Kiswahili.

“Nisamehe mwalimu…nitakupa chochote unachotaka,” alinong’ona mrembo akiwa amesogeza mdomo wake karibu na sikio langu. Nikatabasamu kama kitoto cha mamba, kisha nikalamba midomo hata ungedhani ni mwanamziki anahojiwa. Hoja ya kupewa chochote ilinifurahisha na kunipa matumaini mapya. Hata hivyo, haikutosha kunitoa katika misingi.

Niliichukua karatasi yake ya mtihani na ile ya kujibia, nikaandika vitu fulani, alipoona nilichoandika, machozi yalimbubujika na matone saba yalidondoka haraka, tone la nane nililidaka, kisha nikamwambia, “Simama juu, nisubiri pale nje.”

Mimi na wasimamizi wenzangu tulifanya taratibu zote zinazohusu mwanafunzi aliyevunja sheria za mtihani, ili kubaki na kumbukumbu, nikapiga picha upande mmoja wa majibu aliyoingia nayo yule mrembo, na majibu hayo yalisomeka hivi:

Dhima za Mofimu KI

“Taja dhima tano za mofimu ‘KI’ katika sarufi kisha tunga sentensi mbili kwa kila dhima.”

1.   Hutumika kudogesha

Mifano: Kitoto kinacheza mpira.

Kimeza kimesombwa na mafuriko.

2.   Huonyesha idadi

Mifano: Kijiji kimependezeshwa na bustani za matunda.

Kitabu hiki kinakurasa nne pekee.

3.   Huonyesha upatanishi wa kisarufi

Mifano: Kiatu kimechakaa kama mvaaji wake.

Kiti kimepatikana mtoni.

4.   Kuonyesha mtendwa katika tungo

Anachokipenda kimependwa na wenye nguvu.

Anachokitafuna hana uwezo wa kukimeza.

5.   Kuonyesha kuendelea kwa tendo

Nilipofika kwao alikuwa akicheza.

Alikuwa akisakata dansa bila hofu ya wakwe.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Uhakiki wa Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie